Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt Jabiri Bakari
Na Mwandishi Wetu
Dar es salaam; Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kuwa taasisi ya mfano kwa Mamlaka nyingine za usimamizi wa Mawasiliano barani Afrika zikiwemo mamlaka za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zimekuwa zikifika Tanzania kujifunza kutoka TCRA namna bora ya usimamizi wa sekta ya mawasiliano katika nchi zao.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt Jabiri Bakari akizungumzia ziara ya maafisa wa Mamlaka ya Mawasiliano na Huduma za Posta-Zimbabwe (POTRAZ) waliofanya ziara ya mafunzo katika ofisi za TCRA mwishoni mwa wiki kujifunza namna bora ya usimamizi wa mifumo ya kusimamia masafa ya Mawasiliano, alibainisha kuwa TCRA imeendelea kuwa msimamizi anaetoa ushirikiano thabiti kwa taasisi nyingine za kikanda na kimataifa katika kuhakikisha sekta ya Mawasiliano inasimamiwa vyema, ikizingatiwa kuwa sekta hiyo ni sekta wezeshi wa sekta zote, pia haina mipaka.
“Zimbabwe wamekuja kubenchmark (kujifunza) hapa kwetu, namna tunavyosimamia masafa kwa ustadi; kwa sababu wana mpango wa kupata vifaa bora vitakavyowawezesha kusimamia huduma za masafa kwa ufanisi huko kwao. Kwa kweli Tanzania tumepiga hatua nzuri; tumewapatia mwanga utakaowezesha kuboresha usimamizi wa rasilimali hiyo muhimu,” alisisitiza Mkurugenzi Mkuu Jabiri na kuongeza.
Ufanisi wa TCRA katika kusimamia sekta ya Mawasiliano umetajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizoongeza imani ya Mamlaka nyingine za usimamizi wa Mawasiliano barani Afrika kufika na kujifunza kutoka Tanzania.
Miongoni mwa masuala bayana yanayoiweka TCRA katika ramani ya kuonwa na Mamlaka nyingine za Mawasiliano ilielezwa kuwa ni pamoja na umadhubuti katika usimamizi wa anga la Mtandao uliowezesha Tanzania kuwa kinara kwa usimamizi wa usalama wa anga la Mtandao (wa pili kwa ubora barani Afrika), usimamizi wa rasilimali za Mawasiliano yakiwemo masafa ya Mawasiliano na kuwepo kwa mfumo wa leseni wenye muingiliano wa huduma za Mawasiliano (Converged Licensing Framework) unaotumiwa na TCRA.
Miongoni mwa nchi ambazo zimekuja Tanzania kujifunza namna bora ya usimamizi wa huduma za Mawasiliano kutoka TCRA kwa nyakati tofauti ni pamoja na Mamlaka za Mawasiliano kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Malawi, Zambia, Msumbiji, Zimbabwe na Congo DRC.
TCRA hutumia mitambo jongefu na ya kusimikwa ardhini kusimamia huduma na rasilimali za Mawasiliano ili kuhakikisha anga la Mtandao linatoa huduma za uhakika kwa wananchi. Aidha TCRA hushirikiana na taasisi mbalimbali katika kukamilisha jukumu la usimamizi wa Mawasiliano zikiwemo Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU), Umoja wa taasisi za Mawasiliano Afrika Mashariki (EACO), Shirika la Mawasiliano Afrika (ATU), Umoja wa Posta Afrika (PAPU) wenye makao yake makuu Arusha Tanzania, Shirika la Posta Duniani UPU na Muungano wa Mamlaka za Usimamizi wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA) miongoni mwa taasisi nyingine.






0 Comments