Header Ads Widget

KERO YA BARABARA KATA YA ARUSHA CHINI YAPATA UFUMBUZI.

 


NA WILLIUM PAUL.

WANANCHI wa kata ya Arusha chini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro ambao wamekuwa wakiteseka kipindi cha mvua kutokana na barabara zake kutopitika wanatarajia kuondokana na adha hiyo baada ya Serikali kuanza rasmi kutatua kero hiyo.


Akiuliza swali Bungeni jana, Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini, Prof Patrick Ndakidemi alitaka Serikali kueleza inampango gani wa kujenga daraja katika kata ya Arusha chini litakalounganisha vijiji vya Muungano, Mikocheni na Chemchem.



Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, David Silinde alisema kuwa, katika mwaka wa fedha 2022/2023 barabara hiyo imetengewa Milioni 475 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mto Ronga litakalounganisha vijiji vya Muungano, Mikocheni na Chemchem.


Naibu Waziri Silinde alisema kuwa, mradi huo upo katika hatua za manunuzi kwa ajili ya kumpata Mkandarasi ambapo Serikali kupitia Tarura itaendelea kuweka katika vipaombele vyake ujenzi wa barabara hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuhakikisha inaweza kupitika katika kipindi chote cha mwaka.


Akiuliza maswali madogo mawili ya nyongeza  Mbunge Prof. Ndakidemi alisema kuwa, Barabara ya Getifonga-Mabogini-Kahe iliyopo katika Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa kujengwa kwa kiwango cha lami ambapo huko ndipo inapojengwa hospitali ya wilaya je ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo.


"Swali langu la pili ni barabara ya International school - Kibosho Kncu- Kwa rafaeli imebakiza kilomita 8 kukamilika kwa kiwango cha lami je ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hiyo" alihoji Prof. Ndakidemi.


Akijibu maswali hayo ya nyongeza, Naibu Waziri Silinde alisema kuwa, barabara ya Getifonga-Mabogini-Kahe ipo katika Ilani ya uchaguzi na kwa sasa barabara hiyo ipo katika usanifu kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami.


Alisema kuwa, usanifu unaofanyika ni wa kilomita 31.25 na upo katika hatua nzuri.


Kuhusu barabara ya International school- Kibosho Kncu-Kwa rafaeli kiwango cha kilomita 8.42 kimeshajengwa kwa kiwango cha lami huku sehemu iliyobakia ya kilomita 5.49 na chenyewe wanatafuta fedha ili nacho kijengwe kwa kiwango cha lami.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI