Askofu Mkuu wa Kanisa la AICT Tanzania Musa Masanja Magwesela amesimikwa baada ya kuchaguliwa katika mkutano wa Sinodi kuu ya Kitaifa uliyofanyika mwezi wa tisa mwishoni katika kanisa la AICT Buzuruga Mwanza.
Katika tukio hilo la kuwekwa Wakfu ambalo lilihudhuriwa na Viongozi mbalimbali kutoka Serikalini na watumishi wa Mungu, pia alisimikwa Askofu Mkuu Msaidizi ambaye ni Askofu wa Dayosisi ya Shinyanga Zakayo Bugota.
Tukio la kuwekwa Wakfu kwa Askofu Mkuu na Msaidizi wake lilifanyika katika kanisa la AICT Makongoro kuanza asubuhi saa 2 hadi saa 8 mchana, lilihudhuriwa na umati mkubwa wa waumini kutoka madhehebu mbalimbali Mkoani Mwanza na nje.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali Mgeni Rasmi wa sherehe hizo Waziri wa Madini Dkt Doto Biteko alimpongeza Askofu Mwageswela na Msaidizi wake Askofu Bugota kwa kuaminiwa katika nafasi hizo na kuomba wawaunganishe waumini wa Kanisani hilo ili liendelee kuongezeka kwa idadi ya watu.
"Baba Askofu Mkuu na Msaidizi wake mmeaminiwa sana, mmepewa nafasi ya kumtumikia Mungu na kanisa la AICT Tanzania, fanyeni kazi ya kuhubiri Neno la Mungu kiroho na kimwili ili kanisa hili liwe na maendeleo makubwa" alisema Waziri Biteko.
"Serikali ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan iko bega kwa bega na wewe katika kuwasaidia wananchi wapate kuponywa katika mambo ya kiroho na kimwili maana kanisa lina nafasi kubwa katika maisha ya mtu"
Dkt Biteko alisema anaamini katika uongozi wa Askofu Mkuu Musa Magwesela na Msaidizi wake Askofu Zakayo Bugota, ndio maana wamepewa miaka mingine kuongoza kanisa hilo katika muhula wa pili.
Akitoa salama za kanisa baada ya kuwekwa Wakfu Askofu Mkuu Magwesela alisema wanashukuru sana kupewa nafasi hiyo kumtumikia Mungu na kuomba kupewa ushirikiano ili waweze kutimiza matarajio ya kanisa. Huku akiomba Serikali kutatua migogoro iliyopo kwenye umiliki wa viwanja mali ya kanisa ila kuna watu wanaviingilia kinyemela.
0 Comments