CHAUSIKU SAID,MATUKIO DAIMAAPP MWANZA.
JESHI la Polisi mkoani Mwanza,linawashikilia watu 19 kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili akiwemo mwenye ualbino katika wilaya za Kwimba na Sengerema.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya mauaji ya watu hao wawili kwa nyakati tofauti tofauti katika wilaya hizo ambapo kundi la watu zaidi ya watano walimvamia na kumwua Joseph Mathias Mkazi wa Kwimba na mjane, Getrude Dotto kutoka sengerema.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi, Wilbroad Mutafungwa alisema katika tukio la mauaji lilitokea Novemba 2,mwaka huu, majira ya usiku watu zaidi ya watano wanawashikiliwa wakituhumiwa kumwua Joseph Mathias (28).
Alisema watu hao wanadaiwa siku ya tukio walimvamia na kumshambulia marehemu Mathias (mwenye ualbino), mkazi wa Kijiji cha Ngula wilayani Kwimba,kisha kumkata kwa panga mkono wa kulia na kutokomea kusikojulikana.
Mutafungwa alisema kinara wa mauaji hayo jina linahifadhiwa,alikamatwa Novemba 6,mwaka huu, majira ya saa 6 mchana, katika Kata ya Kanyerere wilayani Misungwi,akiwa na mkono wa marehemu aliokuwa ameuhifadhi kwenye begi jeusi.
“Mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na begi jeusi lililokuwa likitoa harufu ya uozo,baada ya wananchi kumtilia shaka walitoa taarifa jeshi la polisi ambapo alipopekuliwa alikutwa akiwa na kiungo cha binadamu (mkono) akiwa ameuhifadhi ndani ya begi,”alieleza.
Kamanda huyo wa polisi alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa wakati akitafuta mganga wa kumsafisha kutokana na tukio la mauaji,katika mahojiano alikiri kuhusika katika mauaji hayo na mkono huo ni wa binadamu.
Alieleza tukio hilo la kinyama na kikatili limeacha huzuni kwa familia ambapo polisi imejiridhisha kuwa mkono huo ni wa marehemu Mathias ambapo watapeleka sampuli kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupata uchunguzi wa kisayansi.
Kwa mujibu wa Mutafungwa jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa watano huku likiendelea kuwatafuta baadhi waliokimbia na kutahadharisha kila aliyehusika kwenye mauaji hayo hakuna atakayesalimika.
Katika tukio la pili,wanawashikilia watu 14 akiwemo Diwani wa Kata ya Buzilasoga wilayani Sengerema,David Shilinde (62),wakituhumiwa kumwua Getruda Dotto kwa kipigo,kisha kumchoma moto na kubomoa nyumba yake.
Alisema tukio hilo lilitokea Novemba 5, mwaka huu, majira ya saa 2 asubuhi,katika Kitongoji cha Ikonyi B,Sengerema baada ya watu hao kumshambulia marehemu kabla ya kumchoma moto pamoja na kuteketeza nguo zake na wanaye,wakimtuhumu kuiba mihogo.
Mutafungwa alisema chanzo cha mauaji hayo kilisababishwa na baadhi ya ukoo wa marehemu Ndebeye Mihalalo,ambaye alikuwa mumewe Dotto, kuuza shamba hilo la mihogo bila kumshirikisha.
“Marehemu Dotto licha ya kujitetea mihogo hiyo ni mali yake bado watuhumiwa walimshambulia kwa silaha mbalimbali wakiongozwa na diwani wa kata hiyo na mwenyekiti wa serikali ya kitongoji cha Ikonyi B (wote wa CCM),”alisema.
Kamanda huyo wa polisi alisema uchunguzi na upelelezi wa tukio hilo unaendelea na kuwataja watuhumiwa hao kuwa ni Diwani wa Buzilasoga (CCM) David Shilinde (62),Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ikonyi B,Willim Nego,Timuloza Alphonce na Zakaria Meshack.
Wengine ni Zakaria Anthony,Msafiri Jonas,Anthony Medhod,Yusuf Simon,James Mazengo,Emmanuel Makale na Dili Wali na wengine watatu majina yao hayakufahamika mara moja.
Alisema upelelezi wa mauaji hayo unaendelea kabla ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani huku pia msako ukiendelea kuwapata waliotoroka.
Akitoa kauli ya serikali,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima alisema serikali haiwezi kuacha watanzania waishi kwa hofu na mashaka ambapo mkoani humu hataruhusu watu waishi kwa utaratibu huo sababu ya rangi yao wakiwemo wenye ualbino.
“Tukianza kutengeneza albino anaogopa kuishi Mwanza,hilo sitaruhusu na kesi hii iwe fundisho kwa wanaotaka kufanya mauaji ya wenzao,kuna mnyororo hapa na wote tuwapate ili tukomeshe tabia hiyo,” alisema na Malima na kuongeza.
“Maelekezo yangu, sababu zipo nyingi za ovyo ovyo, kila aliyeshiriki kwenye mauaji hayo,akiwemo mganga,aliyeagiza apelekewe mkono wa albino awe mgombea kuwa uteuzi utaniacha,au mchimbaji atapata madini,tunataka tuwajue na hayo mambo wafanye huko na si Mwanza.”
Kuhusu viongozi wa jamii kuhusishwa katika tuhuma za mauaji huko Sengerema,kwa kujichukulia sheria mkononi hatakuwa radhi hadi majibu yapatikane kwa sababu ni ukatili uliopitiliza kutoa uhai wa mtu kwa kipande cha ardhi robo ekari.
0 Comments