Na Hamida Ramadhan Matukio Daima APP Dodoma
JUMLA ya Wasichana 3333 ambao walishindwa kuendelea na Sekondari kutokana na Mazingira magumu,kupata ujauzito na ndoa za utotoni wamefikiwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ambao idadi hiyo ni sawa asilimia 111 ya lengo la Taasisi hiyo
Hayo yalisemwa jijini hapa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dkt,Michael Ng'umbi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Taasisi ya Elimu ya watu wazima(TEWW)ambapo amesema kuwa waliendesha mafunzo kwa nyakati tofauti kwa wasimamizi na watendaji, wawezeshaji na walimu wa madarasa ya mradi wa SEQUIP.
Ameeleza kuwa Taasisi hiyo imehamasisha kurejea shuleni wasichana walioshindwa kuendelea na elimu ya sekondari kupitia vituo 131 vinavyohudumiwa na walimu 803.
Pamoja na hayo Ng'umbi amesema kuwa katika mwaka 2021/2022 TEWW kwa kushirikiana na UNICEF imetekeleza mpango wa elimu changamani kwa vijana walio nje ya shule (IPOSA) ukiwa na vituo 85 vyenye wanufaika 12000 na walimu 290 katika mikoa 9 ya Tanzania bara.
"Mpango huu umelenga maeneo manne ambayo ni stadi za kisomo, stadi za ufundi wa awali,stadi za maisha na stadi za ujasiriamali"amesema
Pia imeendelea kutekeleza programu ya IPPE ambayo ni mpango wa elimu changamani baada ya elimu ya msingi ambao una wanafunzi 842 katika mikoa 11.
Hata hivyo alisema kuwa TEWW itahamasisha, kusajili na kufundisha wanafunzi 3000 wa mradi wa SEQUIP kwa mwaka 2023.
"Lakini pia tunatarajia kupanua mpango wa IPOSA katika mikoa 6 mipya kwa kujenga karakana za kufundishia pia kupanua mafunzo ya tehama kwa wanafunzi wa IPOSA"amesema.
Aidha ametaja vipaumbele vya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/ 2023 kuwa ni pamoja na kuimarisha usajili na usimamizi wa watoa huduma za elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi katika ngazi ya elimumsingi kwa kuboresha mfumo mzima wa usimamizi na ufuatiliaji, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji wa takwimu.
Kuimarisha uendeshaji na utoaji mafunzo kwa walimu na wasimamizi wa elimu ya watu wazima nchini kwa kuboresha mifumo ya tehama.
"Pia kuimarisha uandaaji mitaala, mihtasari na machapisho yanayohusu elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi na kuwa na machapisho bora na kwa wakati.
0 Comments