NA MWANDISHI WETU, Matukio Daima App ZANZIBAR
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, ameeleza haja ya kuwaenzi na kuwathamini wazee, kuwa ni mwendelezo wa utamaduni ulioachwa na viongozi waliopigania ukombozi wa nchi.
Amesema kufanya hivyo ni kujenga ustawi bora wa jamii ya Watu wa Zanzibar.
Othman, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, ameyasema hayo leo Oktoba 2022 kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wazee pamoja na familia mbalimbali alizozitembelea katika ziara yake maalum Visiwani hapa.
Amesema kuwa wazee ni hazina kubwa inayostahiki kuenziwa, kwani kuwepo kwao kunaashiria pia uwepo wa mwendelezo wa hikma, mila, silka, malezi na jamii inayoendelea kulelewa kwa misingi ya maadili kupitia kizazi kimoja kwenda chengine.
“Nasi tunaendelea kujisikia faraja kwa kuona wazee wetu bado mpo; hatunabudi kuendeleza utamaduni wetu wa kupendana na kusaidiana ikiwemo kutembeleana, kwa watu wote, pamoja na wale wenye changamoto mbali mbali”, ameeleza Othman.
Katika ziara hiyo, Makamu huyo wa Kwanza wa Rais, amewatembelea pia Maalim Abdulrahman Bakar Omar ‘Maalim Abouf’, Maalim Suleiman Mohamed Suleiman ‘Babu Sule’ wa Michenzani.
Wengine ni familia ya Bi Amina Awesu, Mzee Talib Kassim wa Monduli na Msomi-Mwanasiasa mashuhuri Zanzibar, Dokta Juma Ameir Muchi wa Mwanakwerekwe, pia Mkoa wa Mjini-Magharibi, Unguja.
Miongoni mwa wazee waliotembelewa katika ziara hiyo ni pamoja na Mzee Hamad Salim (79) Mkaazi wa Magomeni Kwa-Najim ambaye ametoa wito kwa viongozi wa Serikali na vyama siasa kuendelea kujali rika na sehemu hiyo muhimu ya jamii.
Amesema kuwa wazee wa hapa visiwani wameutumia umri wao mwingi katika kupigania Mamlaka ya Nchi bila ya kukata tamaa, hivyo ni wajibu wa viongozi waliopo madarakani sasa, kuendeleza jukumu hilo kwa "kuendelea kutweka tanga hadi pale jahazi litakapofika ufukweni kwa salama na mafanikio zaidi”.alisema.
Masheha na viongozi mbalimbali wa Serikali, Jamii, na vyama vya Siasa, akiwemo Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT- Wazalendo, Salim Bimani, waliambatana na Othman katika ziara hiyo.






0 Comments