Header Ads Widget

RC BABU AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI NA WAFANYABIASHA MKOANI KILIMANJARO.




NA WILLIUM PAUL, MOSHI.


MKUU wa mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amewataka wafanyabiashara na watu mbalimbali kuja kuwekeza katika mkoa huo ikiwamo ujenzi wa viwanda vikubwa kwani Ardhi ipo ya kutosha.


Babu alitoa kauli hiyo alipofanya ziara katika kiwanda cha bia cha Serengeti na kujionea upanuzi wa kiwanda hicho unavyoendelea na kudai kuwa kiwanda hicho ni miongoni mwa viwanda vikubwa katika mkoa wa Kilimanjaro ambacho kimetoa ajira kwa wafanyakazi 800 wakiwamo vijana.



"Uwepo wa viwanda vinavyofanya kazi katika mkoa wetu vinasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana pamoja na kusaidia kukuza uchumi wa wananchi pamoja na Taifa kwa ujumla hivyo niwaite wawekezaji na wafanyabiasha kuja kuwekeza ndani ya mkoa wetu Ardhi ipo ya kutoka kwa ajili ya kuwekeza" alisema Babu.


Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa, kiwanda cha Serengeti ni miongoni mwa viwanda ambavyo huchangia pato kubwa la Taifa kwa kulipa kodi kubwa huku mwaka wa fedha 2021/2022 walilipa kodi ya Bilioni 201.



Alisema kuwa, uendelezaji wa kiwanda hicho ni muhimu kwani utaongeza ajira kwa vijana pamoja na wakulima wa zao la Shairi ambao wamekuwa wakiwauzia nafaka hiyo.


Aidha Babu alifurahishwa na jinsi ambavyo kiwanda hicho kimekuwa kikijitoa kuisaidia jamii katika ujenzi wa miradi mbalimbali kutoka na ile faida wanayoipa.



Katika hatua nyingine Babu alitoa wito kwa uongozi wa kiwanda hicho kujenga mahusiano mazuri na wafanyakazi wake na kuepuka tabia ya kuwanyanyasa kwani kufanya hivo ni kukiuka sheria na taratibu za nchi.


Naye Mkurugenzi wa mawasiliano wa kiwanda hicho, John Wanyancha alisema kuwa, kwa sasa wanaendelea na upanuzi wa kiwanda hicho lakini changomoto kubwa wanayokutana nayo ni ufinyu wa Ardhi na kumuomba Mkuu wa mkoa kuwasaidia kupata eneo linalomilikiwa na Serikali lililopakana na kiwanda hicho.



"Tumekuwa tukiendelea na shughuli za upanuzi wa kiwanda ili kuzalisha pombe kali lakini tunalo tatizo la uhaba wa Ardhi tunakuomba utusaidia tuweze kupata eneo tulilopakana nalo ambalo ni la Serikali na halitumiki kwa chochote tuweze kufanya upanuzi mkubwa" alisema Wanyancha.


Mkurugenzi huyo alisema kuwa, asilimia 80 ya nafaka inayotumiwa na kiwanda hicho hutokea kwa wakulima wa Tanzania kutoka mikoa nane ambao huuza mazao yao katika kiwanda hicho na kudai kuwa kupanuka kwa kiwanda hicho utaongeza fursa kubwa kwa wakulima na vijana.


Aidha alisema kuwa, kutoka na faida wanayoipata kiwanda hicho wamekuwa wakishiriki katika shughuli za kuisaidia jamii katika ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwamo uchimbaji wa visima vya maji, kuwafundisha wananchi madhara ya kunywa pombe kupita kiasi, kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaosomea Ugavi pamoja na upandaji miti katika maeneo mbalimbali nchini.



Wanyancha alisema kuwa, kiwanda hicho ni miongoni mwa walipakodi wakubwa na kila mwaka Kodi imekuwa ikiongezeka na mwaka 2021/2022 kiwanda cha Serengeti kililipa Bilioni 201 kama Kodi mbalimbali.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI