Header Ads Widget

NYUMBA 14 ZIMEKAMATWA KWA KUIBA UMEME ZANZIBAR

 


Na MWANDISHI WETU,ZANZIBAR - MATUKIO DAIMA APP

Waziri wa Maji, Nishati na Madini Shaibu Hassan Kaduara amezibaini nyumba  14 za makazi ya watu wanatumia umeme kinyume na sheria kwa kutengeneza njia maalumu ya wizi kwenye mita au kuunga moja kwa moja kutoka kwenye waya mkubwa wa umeme hali ambayo inapelekea hasara kwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).


Nyumba hizo zimebainika maeneo ya Mazizini, Chukwani na Mbuyu Mnene kupitia zoezi maalumu lililopewa jina la Kaduara Operesheni ambalo lina lengo la kuwafungia watu mita pamoja kuwasaka watu wanaotumia umeme kinyume na sheria katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.


Akizungumza na waandishi wa Habari,eneo la Mbuyu Mnene Unguja mwishoni mwa wiki iliyopita Mhe Kaduara alisema ZECO inapoteza umeme kwa njia kama hizo ambazo watu wanatumia umeme kinyume na sheria hivyo wote waliyobainika wanatumia umeme kinyume na sheria  watatozwa fidia kwa sababu ni kosa la kuhujumu uchumi wa nchi.


Alifahamisha   hesabu maalumu zitatumika katika kuwatoza fidia kutokana na vitu vya umeme ambavyo wahusika wamekutikana navyo na muda utakisiwa si chini ya mwaka mmoja. Asilimia 40 ya umeme unapotea kwa njia kama hizo za watu wanaiba umeme, hivyo hatamuonea mtu huruma.  


“Ndani ya siku mbili nimezikamata nyumba 14 zinatumia umeme kinyume na sheria, wako ambao wamezifungua mita za umeme na kutengeneza ujanja wa kuiba umeme, “by pass” wengine wameunga kupitia waya mkubwa wa umeme na kuingiza ndani ya nyumba zao, wote hao wana matumizi makubwa ya vitu vya umeme ! sitomuonea mtu muhali  watalipa fidia ” Alisema Kaduara.


Mapema Waziri huyo alizungumza na wafanyakazi wa ZECO katika kiwanja cha ofisi hiyo Saateni, Unguja na kuwaeleza kwamba mfanyakazi yeyote atayebainika ameshiriki kuwaungia wananchi umeme kinyume na sheria atamfukuza kazi kwasabau alitoa taarifa kwa muda wa mwezi mmoja kwamba kama kuna mfanyakazi alijihusisha na kosa hilo ajitokeza huenda akamsamehe lakini hakuna aliyejitokeza.


Alieleza kwamba anayo baadhi ya majina ya wafanyakazi ambao wanatuhumiwa kushiriki kuwaungia watu umeme kinyume na sheria hivyo atawafukuza kazi kwasababu yeye hayuko tayari kutenguliwa katika uongozi kwa kuwalinda  watendaji wa ZECO kwani watendaji hao walimuahidi watamsaidia lakini ameona hawamsaidii kutokana na malalamiko mengi dhidi ya shirika hilo.

Aidha aliagiza uongozi wa ZECO kuwalipa haki zao wafanyakazi waliyorudishwa kazini baada ya kusimamishwa kazi. Alisema wafanyiwe hesabu na walipwe haki zao zote kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa Umma.


Kwa Upande wake katibu Mkuu wa Wizara hiyo Joseph Kilangi ametoa wito kwa wananchi wanaotaka kuungiwa umeme wampigie simu moja kwa moja endapo mtumishi wake wa ZECO atawaomba fedha kwa nia ya rushwa. Hivyo amewata wapige simu nambari 0777420741.


 Alisema hakuna sababu ya wananchi kutoa pesa kinyume na sheria kwa nia ya kufikishiwa huduma ya umeme.

Pia alihimiza nidhamu za kazi kwa watendaji hao na kusema kwamba nidhamu ya kazi inaanza na mahudhurio ya kazi  kufika kazini mapema, kuacha utoro, kufanya kazi kwa mashirikiano pamoja kuwajibika ipasavyo ili kupunguza malalamiko kwa wananchi.


Naye Fundi Mkuu wa ukaguzi umeme ZECO Juma Mussa Omar alisema kila chombo kilichopatikana ndani ya nyumba ambayo watu wanatumia umeme kinyume na sheria kimeorodheshwa hivyo hesabu ya fidia itafanywa kwamujibu matumizi ya vyombo vya umeme vilivyopatikana ndani nyumba hata kama hakitumiki.


Zoezi maalum la kuwafungia wananchi mita na kuwakamata watu wanaotumia umeme kinyume na sheria (Kaduara Uperesheni) limewashirikisha viongozi wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini (WMNM) akiwemo, waziri wa Maji  Kaduara, Naibu waziri Shabaan, Katibu Mkuu Kilangi, Naibu katibu Mkuu Mwanjuma, wakurugenzi, fundi Mkuu wa ukaguzi umeme ZECO, Maafisa wa ZECO, Afisa Uhusiano WMNM, Sheha wa eneo husika na vyombo vya ulinzi na Usalama.









Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS