NA HAMIDA RAMADHANI,DODOMA
KATIKA miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na kasumba kwa baadhi ya wanawake wenye watoto wadogo kuwaachisha kunyonya mapema watoto wao kabla ya kufikisha miaka miwili.
Hii ni kwa kuhofia matiti kulala huku wengine wakidai ni kutokana na majukumu ya kikazi.
Hali Kama hii inaelezwa kusababisha taifa kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye udumavu wa mwili na akili.
Tatizo hili linaonekana kuwa kubwa na limekuwa likidhoofisha maendeleo ya nchi hii husababishwa na kutokuwa na uhakika wa chakula, uboreshaji wa elimu ya afya bora ya mama na mtoto hapa nchini.
Lishe duni na kutonyonyesha watoto kwa muda wa miaka miwili pia ni miongoni mwa sababu kubwa ya vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano, hivyo inakadiriwa kugharimu serikali asilimia 2.6 ya pato la taifa.
Mara nyingi, udumavu huwakumba watoto walio chini ya miaka mitano, na hutokea pale mtoto anaposhindwa kupata lishe bora tangu akiwa tumboni kwa mama yake na siku 1,000 za mwanzo wa uhai wake.
Wataalamu wa masuala ya lishe wanaongeza kusema kuwa, tatizo hilo pia linaweza kutokea kwa mtoto katika kipindi cha mwaka wa kwanza, wa pili na hadi anapofikia umri wa miaka mitano.
Lakini pia hali hiyo inaweza kutokea endapo mtoto hatopata lishe bora ambayo inahusisha kunyonya maziwa ya mama kwa muda wa miezi sita ya mwanzo bila kumchanganyia na chakula chochote na kuendelea kunyonyeshwa hadi anapofikisha miaka miwili.
Baadhi ya nyakati, kina mama hukumbana na changamoto ya mtoto mwenyewe kukataa kunyonya, hivyo mzazi kulazimika kumpa chakula tofauti na maziwa na hatimae kukosa vile virutubisho muhimu katika ukuaji wa mtoto.
Mtoto anapofikisha umri wa miezi saba anatakiwa kupata chakula mchanaganyiko na akitimiza mwaka mmoja anatakiwa kupatiwa vyakula bora kwa sababu mahitaji yake yanaongezeka huku akiendelea kunyonya ziwa la mama
Elieth Deogratius Rumanyika ni Afisa Lishe kutoka Wizara ya Afya anasema kuna viwango vya ukuaji vinavyopimwa kwa mtoto ili kugundua kama ana udumavu au la.
Rumanyika anaeleza kuwa katika hatua ya kwanza, mtoto anapimwa akiwa na umri wa mwaka mmoja ambapo wataalamu wa afya na lishe wanasema mtoto katika umri huo angalau awe na kilo 10 na urefu unaolingana.
"Kwani hata mama anapohudhuria kliniki kadi inaonyesha kuna rangi nyekundu inaonyesha mtoto yuko kwenye hatari, rangi ya kijivu anakaribia kufika kwenye hatari na mtoto anapofikia kwenye kijani maendeleo yake yako vizuri," anasema Rumanyika.
Anaongeza, "Kama ikatokea mtoto kila akipimwa uzito wake unaangukia kwenye kijivu au nyekundu, basi mtoto atakuwa na uzito pungufu na msaada wa haraka utahitajika na mama anatakiwa kushauriwa vitu vya kuzingatia ili uzito wa mtotouongezeke."
“Mtoto mwenye udumavu wa akili ni yule aliyekosa lishe bora ikiwemo kunyonya maziwa ya mama yake ipasavyo na anakuwa hana utambuzi kwa baadhi ya mambo vitu picha na vitu vya rangi mbalimbali ingawa kuna watoto wanaozaliwa na changamoto hiyo," anabainisha Rumanyika.
JITIHADA ZA SERIKALI .
Afisa lishe huyo anasema serikali imetoa motisha kwa akina mama kwa kutoa likizo ya uzazi kwa muda wa miezi sita ambapo lengo ni kuhakikisha kuwa kina mama hao wanapata muda mzuri na wa kutosha kukaa na watoto wao na kunyonyesha ipasavyo.
Pia amesema baada ya kumaliza likizo hiyo ya uzazi kwa kipindi hicho cha miezi sita, mama anaye nyonyesha na akiwa mtumishi wa serikali anaruhusiwa kufanya kazi nusu siku lengo likiwa ni kuhakikisha mtoto anapata maziwa ya mama kwa wakati na ya kutosha ili kudhibiti tatizo hilo la udumavu kwa watoto.
Adella Mlingi ni Kaimu Afisa Lishe Mkoa wa Dodoma anasema hali ya lishe hairidhishi mkoani humo.
Kwa mujibu wa Adella, takwimu zilizotolewa na Taasisi ya Lishe na Chakula Tanzania (TFNC) mwaka 2018 zinaonesha udumavu mkoani Dodoma upo kwa asilimia 37.2, hii ikimaanisha, katika kila watoto 100, watoto 37 wamedumaa.
Pia takwimu hizo hizo, zinaonyesha kwa mwaka 2018, kulikuwa na watoto chini ya miaka mitano 433,576 ambapo 37.2% ya hiyo ni sawa na watoto 161,290.
Anasema hata hivyo, mkoa umejiwekea mikakati ya kupunguza udumavu kwa kuendelea kutoa elimu kwa wanawake ili kuhakikisha wana kuwa na hali nzuri ya lishe wakati wa ujauzito na wakati wa kunyonyesha baada ya kujifungua.
Pia wanaendelea kuelimisha kina mama kuhakikisha watoto wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee, bila kupewa maji, vinywaji au vyakula vyengine katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa.
"Mikakati mingine ni kuhakikisha watoto wenye umri wa miezi 6 – 23 wanapewa vyakula vya nyongeza vyenye ubora kilishe," anasema.
"Mikakati mingine ni kuwapatia kina mama wajawazito vidonge vya kutosha vya madini chuma kwa ajili ya kuongeza wingi wa damu kipindi chote cha ujauzito,” na kuongeza "Bila kusahau kuwapatia watoto wenye umri chini ya miaka mitano matone ya vitamini A na dawa za minyoo."
Msimamo wa kina mama kuhusu kunyonyesha miaka miwili
Saida Khamisi ni mama aliyenyonyesha mtoto wake kwa muda wa miezi sita tu ambapo anasema yeye alipenda kumuachisha mwanae ili aweze kujitegemea na kuweza kula vyakula mchanganyiko bila kusumbua na hiyo yote nikutokana na majukumu yake ya kazi.
"Nikweli jamii ilinishangaa lakini nilihakikisha mwanagu anapata lishe bora inayo imemjenga mpaka leo hii anapokwenda kutimiza mwaka mmoja," anasema.
Alipoulizwa juu ya athari za kuachisha mapema hali inayopelekea mtoto kupata udumavu wa akili anaeleza kuwa udumavu unatokea pale mtoto anapokuwa hajapata ziwa la mama yake vizuri na usipozingatia lishe bora.
"Sasa kama mimi nimemuachisha mwanangu akiwa na umri wa miezi sita, lakini nahakikisha anapata lishe bora kutoka kwenye makundi yote ya vyakula," anaeleza.
"Mtoto kupata udumavu kunasababishwa na lishe mbovu lakini kama mtoto anapewa lishe bora hawezi kupata udumavu," anasema.
‘’Niwashauri wazazi wenzangu kama kuna shida, na kuna ulazima wa mtoto kuachishwa mapema, basi wazingatie lishe bora kwa watoto ili kuepuka tatizo la udumavu, ’’anasema Saida.
Naye Mwanaidi Japhari ambae ni mama wa watoto wawili anaeishi Maili Mbili jijini Dodoma, anasema yeye ameweza kuwanyonyesha watoto wake wote kwa muda wa miaka miwili ambapo kwa kipindi cha miezi sita aliweza kuwanyonyesha wanae maziwa yake pekee bila kuchanyanya chakula chochote.
Anasema baada ya miezi sita ndipo alipoanza kuwapa chakula mchanganyiko na kutoka kwenye makundi yote ya vyakula kama yanavyofahamika.
”Kutokana na elimu tunayopata pindi tunapokwenda kliniki, ni muhimu kunyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee,” anashauri Mwanaidi.
Mwanaidi anasema hiyo imewaepushia watoto wake kuugua mara kwa mara na vigonjwa vya ajabu ajabu.
Hamasa kwa wadau
Wadau wameendelea kutoa hamasa kwa kuhakikisha unywaji wa maziwa mashuleni hasa katika shule za msingi.
George Msalya ni Msajili wa Bodi ya Maziwa anasema kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa ya watoto wenye udumavu hapa nchini, ndio maana imetengwa wiki maalumu ya hamasa ya unywaji maziwa mashuleni.
Tafiti zinaonyesha kwamba, baadhi ya watoto wanaenda shule asubuhi bila kunywa chai nyumbani.
“Hii ina maana, watoto hawa tangu walipokula jana hawatapata chakula tena mpaka watakaporudi nyumbani saa nane hadi saa tisa mchana,Ukweli ni kwamba, kwa watoto hiki ni kipindi kirefu kukaa bila kula na hali hiyo husababisha watoto kuchoka haraka na kuanza kusinzia na hivyo kukosa mafunzo wanayopewa na walimu wao,” anasema msajili huyo.
Na kuongeza “Wataalam wa lishe wanashauri chakula anachopewa mtoto kiwe na viini lishe vyote vinavyotakiwa kwenye chakula bora yani kiwe na wanga, protini, mafuta, vitamini madini na maji ya kutosha na ili upate chakula cha namna hiyo ni lazima kuchanganya na kuhitaji maandalizi marefu.
Hivyo wataalamu wa lishe wanashauri ukipata glasi moja ya maziwa katikati ya siku basi utakuwa umepata lishe ya kumtosha hadi atakaporudi nyumbani,” anasema msajili huyo.
Anasema ndio maana zaidi ya nchi sabini duniani zimeshaanza mpango wa maziwa shuleni kwa watoto wao.
Ushauri
Wazazi wenye watoto wanashauriwa kutambua kuwa hakuna kitu kizuri kama kuwezekeza kwenye afya ya mtoto.
Wataalamu wanasema kuna tofauti kubwa kati ya mtoto aliyepata lishe bora na yule aliyekosa.
”Wazazi tumekuwa tukiwekeza kwa watoto wetu kwenye mambo ambayo sio ya msingi, na kusahau lishe za watoto wetu hivyo tunatoa wito wazazi tuwekeze nguvu kubwa kwa watoto wetu hasa kwenye suala zima la lishe,” anashauri George.
Hata hivyo serikali, imechukua baadhi ya hatua kwa lengo la kupunguza tatizo hilo.
Hivi karibuni rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, pamoja na waziri wa Afya Ummy Mwalimu wametia saini mkataba wa usimamiaji shughuli za lishe kwa maslahi ya Taifa.
0 Comments