Header Ads Widget

UTT - AMIS WAKWEA MLIMA KILIMANJARO KUCHAGIZA UTALII WA NDANI



Na. Calvin Katera.


Jumla ya Watumishi 22 kutoka Taasisi ya Mifuko ya Uwekezaji nchini (UTT-AMIS), wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Faustine Kamzola na watumishi wengine wawili kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) wameanza safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia lango la Marangu leo Machi 23, 2026 kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani ulioasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia filamu yake ya Tanzania The Royal Tour.

Akiwaaga wapanda mlima hao 24, Mkuu wa Wilaya ya Moshi mjini  Mhe. Godfrey Mzava alisema kuwa UTT-AMIS na NDC kwa kupanda Mlima Kilimanjaro wamekuwa mfano kwa taasisi na makampuni mengine kujitangaza na kushiriki utalii wa ndani kwa kutembelea vivutio mbalimbali nchini.

Aidha Mhe. Mzava alisema "kupitia kampeni hii waliyoifanya UTT-AMIS na NDC ya kupanda Mlima Kilimanjaro niwahamasishe na taasisi nyingine za umma na mashirika binafsi kuja kupanda Mlima Kilimanjaro. Kupanda kwenu kutaliongezea Taifa mapato”.

Vilevile, Mhe. Mzava alisisitiza kuwa ulinzi wa Mlima Kilimanjaro siyo jukumu la TANAPA tu bali nila kila mwananchi anayepakana na hifadhi hiyo kwakuwa ulinzi shirikishi baina ya jamii na hifadhi hulinda usalama wa maliasili zilizomo.

Naye, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro - Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Angela Nyaki alisema kuwa kwa kipindi walichokichagua UTT-AMIS na NDC kupanda mlimani ni kipindi kizuri, kwani kipindi cha mvua kama hiki mlima unakuwa na oksijeni ya kutosha na ni matarajio ya wengi nasi wahifadhi tukiwemo kuona wageni wote 24 wanafika kileleni.

Hata hivyo, Kamishna Nyaki aliwahakikishia kuwa kwakuwa kipindi hiki ni cha mvua, hifadhi imejiandaa kufuatilia safari yao kuanzia wanapopanda hadi watakaposhuka ili kuhahakikisha wageni wote wanafurahi kuwepo hifadhini sanjani na kufikia malengo mama ya safari yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya UTT-AMIS Prof. Faustine Kamzola alieleza kuwa sababu za kupanda Mlima Kilimanjaro ni nyingi mno kwa kila mgeni lakini kubwa zaidi kwao ni kuimarisha afya na tiba ya mwili.

Pia, aliongeza kuwa zoezi hili la kupanda mlima ni maandalizi ya kuuanda mwili na akili kwaajili ya kupanda mlima ifikapo tarehe 9 desemba 2026, siku ambayo watanzania wengi na wageni kutoka mataifa mbalimbali hujumuika kwa pamoja kupanda Mlima Kilimanjaro kusherekea siku ya Uhuru wa Tanzania bara uliopatika desemba 09, 1961 kwa kupandisha Bendera ya Taifa katika kilele hicho.

Kundi hili la watumishi wa UTT-AMIS na NDC wanatarajia kutumia siku sita katika safari hiyo iliyoanza leo Machi 23, 2026 ikiwa siku ya kwanza watalala katika kituo cha Mandara kuelekea kilele cha Uhuru chenye urefu wa Mita 5895 kutoka usawa wa bahari.







Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI