NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Prof. Patrick Ndakidemi ameshiriki maadhimisho ya siku ya wazee duniani kama mgeni rasmi katika viwanja vya Radio Kicheko mkoani Kilimanjaro.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wazee kutoka sehemu mbalimbali za mkoa wa Kilimanjaro ambapo walishiriki katika michezo mbalimbali, kucheza ngoma za asili na dansi na kujipatia chanjo za UVIKO 19 kwa waliohitaji.
Akimkaribisha Mbunge katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Redio Kicheko Live Dr Heavenlight Kavishe alimshukuru Mbunge kwa kukubali kushiriki nao, na kuwa mmoja wa wafadhili wa shughuli hiyo pamoja na kuwashukuru wazee kwa mwitikio mkubwa na ushiriki wao katika siku hiyo muhimu ya wazee duniani.
Dr. Kavishe ameiomba Serikali kuangalia kwa jicho la kipekee masuala ya wazee kwani wanakabiliana na changamoto nyingi na kubwa ikiwa ni swala la kutokuwa na bima za Afya.
Wakiongea kwa nyakati mbalimbali, wazee waliohudhuria katika maadhimisho hayo walilalamika kutokuwepo kwa dirisha maalum la wazee katika mahospitali, vituo vya afya na zahanati.
Pia wazee walieleza changamoto ya bima zao za afya kutokidhi vigezo vya kupatiwa huduma zote huku kero ingine iliyowasilishwa ni kusitishwa kwa bima za CHF ambazo wazee wengi vijijini walikuwa wanazimudu kutokana na unafuu wake na kuiomba Serikali kuangalia masuala hayo ya afya kwa jicho la pekee.
Kero ingine iliyowasilishwa na mama Dativa Lyimo iliainisha kuwa wale waliostafishwa kwa sababu za ugonjwa kama vile kupata ulemavu wakiwa kazini, hawapewi mikopo ya halmashauri ya asilimia 2 kama walemavu wengine. Alishauri ni muhimu watu hawa wapewe mikopo katika kundi la walemavu.
Mzee Wenseslaus Aloyce alisema kuwa Serikali imewasahau wazee kabisa na hawapewi mikopo kama watu wengine kwenye makundi maalumu. Aliomba wazee nao wapewe mikopo kama makundi ya akina mana, vijana na walemavu.
Katika maadhimisho hayo, wazee walionyesha masikitiko yao kutokana na kuporomka kwa kasi kwa maadili ya vijana wetu. Walieleza kuwa vijana wengi sasa hivi hawataki kufanya kazi, na baadhi wamekuwa walevi wa kupindukia. Baadhi ya vijana wanatumia pombe kali na bangi.
Mama Martha Lyaruu alilalamikia kero ya wazee kutoka kaya maskini kutokuwekwa kwenye mpango wa TASAF.
Alisema, baadhi ya maeneo fedha hiyo hutolewa kwa upendeleo kwa watu wasio na vigezo.
"Kuna wanaopata fedha ya TASAF lakini hawastahili kupewa kwani hawajakidhi vigezo lakini wanawekwa katika mpango wa TASAF" alisema Mama huyo.
Aliiomba Serikali ifuatilie na haki itolewe kwa wazee wasio na uwezo.
Akijibu hoja za wazee, Mbunge Ndakidemi aliwahakikishia kuwa kero zote ambazo wamezitoa atazifikisha kwenye mamlaka husika ikiwa ni pamoja na maswala ya Bima ya Afya kwa wazee, TASAF kwa kaya maskini pamoja na mambo yote yaliyoibuliwa yanayohusu kero za wazee kwa ujumla.
Mbunge aliwaomba wazee watumie mamlaka yao ya uzee kuwafunda vijana ili wajirekebishe kimaadili na kumshauri wazee washirikiane na taasisi za dini ili kufanikisha swala la maadili kwa vijana.
Mbunge alimshukuru Mkurugenzi wa Redio Kicheko live kwa kuandaa tamasha na kuwathamini wazee, kwani wazee ndiyo urithi na hazina yetu. Vilevile aliwashukuru wazee kwa kujumuika katika tamasha hilo na kubadilishana mawazo.










0 Comments