Header Ads Widget

WADAU WAUNGA MKONO SERIKALI MAPAMBANO YA KICHAA CHA MBWA

 


Wadau wa ustawi wa Wanyama  wa Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na ustawi wa Wanyama nchini Tanzania linalojulikana kama Education for African Animals Welfare (EAAW) na Meru animals Welfare (MAWO) wameendelea kuiunga  serikali mkono katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Akizungumza kwa niaba ya wadau hao, Mkurugenzi  wa EAAW Bw. Ayubu Nnko amesema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana na Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida kwa kutoa chanjo ya kichaa cha mbwa Pamoja na matibabu,wakihudumia Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.

Nnko ameeleza kuwa mwaka huu walizindua maadhimisho hayo siku ya tarehe 23 Septemba katika Kijiji cha Yulansoni na Msingi kata ya Kinyangiri Wilaya ya Mkalama, ambapo mpaka sasa zaidi ya Mbwa 518 na Paka 29 wamekwishakupatiwa chanjo na zoezi hilo litaendelea kutolewa  ambapo wanategemea wanategemea kuhusisha vijiji vya Nduguti na Maziliga ,naisinyai,Naepo ,mererani, Shambarai na Olkersmet.


Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho hayo katika Wilaya ya Mkalama Kijiji cha Yulansoni, Daktari wa mifugo wilaya ya Mkalama Elias Mbwambo amelishukuru  EAAW na kusema kuwa shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Wilaya ya Mkalama bega kwa bega katika mapambano dhidi ya kichaa cha mbwa.


 Sambamba na hayo ameitaka jamii kutoa ushirikiano pale wanapoletewa chanjo na kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katika matunzo ya mbwa na paka ili kuepusha madhara.


Kwa upande mwingine Mbwambo ameeleza kuwa Mbwa wamekuwa wakifugwa na binadamu tangu ustaarabu ulipoanza na wanafugwa kwa malengo mbalimbali yakiwemo ulinzi, kuchunga mifugo, uwindaji.


 Zaidi ya asilimia 98 ya mbwa wanaofugwa nchini ni wa asili (mongrel) na mbwa wachache ni wa kisasa ambao hufugwa zaidi maeneo ya mjini. Amesisitiza kuwa Mbwa kama mifugo wengine wanatakiwa kupatiwa huduma zote za msingi kama chakula, maji, matibabu, malazi na kuogeshwa kwenye dawa za kuua wadudu. Kulingana na Sheria za Tanzania, mbwa hatakiwi kuachwa akitembea mitaani.


 Halikadhalika amewatahadharisha wafugaji kuhakikisha kuwa, mbwa wanafungwa kwenye banda au mnyororo muda wote wa mchana. 


Kwa mbwa wanaotumika kwa kazi za kuchunga mifugo au kuwinda, ni vema wakawa chini ya uangalizi wa mwenye mbwa ili wasidhuru watu wengine; Pia ni  vyema mbwa akapata mafunzo ya msingi ili aweze kutii amri ya anaemmiliki ili kuepusha madhara.



"Ni Dhahiri kuwa kuna madhara mbalimbali yanayotokana na kutokuzingatia ufugaji bora wa mbwa. Madhara hayo ni Pamoja na Kung`ata na kujeruhi watu au mifugo mingine hivyo kupata kesi na  Kusababisha hofu na kuwa tishio kwa jamii na Kueneza magonjwa kama vile kichaa cha mbwa na tegu wa mbwa"Alisema.



 Kichaa cha mbwa huambiza kwa njia ya kung’atwa na mbwa mwenye ugonjwa huo. Binadamu pia anaweza kuambukizwa kwa kugusa mate ya mbwa mwenye kichaa. 


"Dalili za ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni Pamoja na Mbwa kubadilika tabia, ama kuwa mkali au mpole kuliko ilivyo kawaida, Mbwa kushindwa kula, kukwepa maji na kupooza miguu ya nyuma, kudondosha mate mengi na ulimi kuning’inia nje ya mdomo, Kubweka mara kwa mara  na kukitoa mlio usio wa kawaida"Alisema



Akihitimisha Mkurugenzi wa EAAW amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa jamii hasa kwa maeneo ya vijijini kushirikishwa kwa kiasi kikubwa katika tafiti na uenezwaji wa elimu juu ya matunzo ya Wanyama, kwani kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kwa serikali na wadau mbalimbali kutatua matatizo yanayowakabili wananchi na sekta ya mifugo.



Hata hivyo amevitaka vyombo vya Habari kushiriki zaidi katika kutangaza shughuli zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza sekta ya mifugo, ustawi wa Wanyama na jamii kwa ujumla. Kilele cha maadhimisho ya kichaa cha mbwa hufukiwa terehe 28 ya kila mwezi wa septemba duniani kote.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI