Header Ads Widget

MBUNGE NDAKIDEMI AKUTANA NA WAJUMBE WA HALMASHAURI KUU CCM KATA YA OLDMOSHI MAGHARIBI KATIKA JIMBO LA MOSHI VIJIJINI

 



NA WILLIUM PAUL, MOSHI.

Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Ndakidemi amezungumza na viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi wa Kata ya Oldmoshi Magharibi kwenye kikao cha kazi kilichofanyika katika eneo la Kiboroloni.


Akizungumza na viongozi hao wa Chama, Mbunge alianza kwa kuwapongeza kwa kuchaguliwa kwao kushika nafasi katika ngazi ya matawi, kata, Wilaya  na jumuiya za chama.



Aliwaomba  waimarishe upendo na mshikamano baina yao na viongozi wa kisiasa na serikali sambamba na kuwaomba wazidi kuiunga mkono Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kutetea kwa nguvu zote kazi kubwa zinazotekelezwa na serikali kutatua kero za wananchi wa Tanzania. 


Kwenye mkutano huo, Mbunge aliwaomba viongozi hao wawe mabalozi kwenye kuelezea umma kazi nzuri za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali yao ya CCM iliyoko madarakani ambayo wameipigania.



Diwani wa Kata hiyo, Super Macha alieleza miradi yote ambayo imetekelezwa na Serikali tokea uchaguzi wa 2020 ulipokamilika. 


Miradi hiyo ni pamoja na ule wa maji wa Tela Mande uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 905 na kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.  



Wajumbe wa mkutano huo waliridhika kwa kiwango kikubwa kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi katika Kata ya Oldmoshi Magharibi.  


Waliomba wapatiwe nakala za ripoti hiyo ili wakawe mabalozi wa kuelezea uma kazi kubwa iliyofanywa na Serikali na Mbunge na Diwani waliahidi kuandaa na kuwapatia nakala za kutosha.


Walipopewa fursa, viongozi hao walimweleza Mbunge changamoto ambazo zinawakabili wananchi ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi. 


Baadhi ya kero ambazo ziliwasilishwa kwenye mkutano huo ni pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara kama ile ya Kiboriloni - Mande - Tela;  Mungureni - Mande; na Sango - Mandaka Mnono. 


Kero nyingine kubwa ni ile ya wafugaji kupeleka mifugo katika mashamba ya mpunga katika kijiji cha Mandaka Mnono na kulisha mifugo mazao yao.


Walilalamika kwamba kero hiyo bado haijapatiwa suluhu na mamlaka za wilaya huku upande wa akina mama, kero yao  kubwa ni ya ukosefu wa maji safi na salama kwenye kijiji cha Mandaka Mnono.


Akizungumza wakati wa kujibu kero ambazo ziliwasilishwa na baadhi ya wajumbe katika mkutano huo kwa niaba ya wananchi wa Oldmoshi Magharibi, Mbunge alisema kuwa kwa upande wa ubovu wa miundombinu ya barabara, ataendelea kulifanyia kazi kwa kushirikiana na Diwani na viongozi wengine wa serikali.


Alisema kuwa kama walivyofanya hapo awali kwenye baadhi ya maeneo korofi ambapo barabara zilitengenezwa, na makalavati kuwekwa kwenye sehemu korofi, na kudadabua mito iliyokuwa inaharibu barabara. 


Aliwahakikishia wajumbe kuwa kero zote ambazo zimewasilishwa atazitafutia ufumbuzi, kama alivyofanya kwenye utatuzi wa kero zingine hapo awali ambazo zilikuwa changamoto kubwa kwa wananchi. 


Ndakidemi aliwashukuru sana viongozi wote wa Chama cha Mapinduzi kata ya Oldmoshi Magharibi kwa kufanya naye kazi na Diwani kwa ushirikiano, katika kuhakikisha wanatekeleza ilani ya chama hicho kwa vitendo, na kuhudumia wananchi ipasavyo kwa kuwatekelezea miradi mbalimbali ya maendeleo kama walivyo ahidi kipindi cha kampeni kwenye uchaguzi mkuu 2020.


Wakati wa kuhitimisha ziara ya Mbunge, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Oldmoshi Magharibi, Godson Mchau alimpongeza Mbunge kwa kutenga muda wake na kuja kusikiliza kero za wananchi ili zitafutiwe ufumbuzi.


 Aliahidi ushirikiano kwa Mbunge na Diwani wakati wakitekeleza majukumu yao ya kisiasa.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI