Header Ads Widget

KUMBUKIZI YA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE-- TOKA MWAKA 1922 HADI MWAKA 1999.

 





BABA wa taifa , Mwalimu Nyerere hayupo nasi tena ,Rabuka muumba amemuita baada ya maisha yake duniani kuanzia alipozaliwa April 13 mwaka 1922 hadi yalipomalizika Oktoba 14 mwaka 1999. Nyerere ambaye wengi hivi sasa bado wanamkumbuka na kumlilia ,alizaliwa Mashariki mwa ziwa Victoria katika kijiji cha Butiama ,Wilaya ya Musoma vijijini ,mkoani Mara.


Mwalimu alizaliwa katika kabila dogo la Wazanaki ambalo ni moja ya makabila 26 madogo madogo yaliyoko Mara, Baba yake Nyerere Mzee Burito alifariki mwaka 1942, alikuwa Chifu wa kabila Wazanaki. Mama yake Mugaya Nyang'ombe aliyekuwa pia Mzanaki alifariki mwaka 1998 akiwa na umri wa miaka 105.


Alipokuwa kijana mdogo Nyerere alifanya kazi kama kuchunga ng'ombe pamoja na kilimo ambapo mara nyingi mlo wake ulikuwa mara moja kwa siku. Wakati alipokuwa akichunga ng'ombe Nyerere alisikia habari za Shule ambazo aliambiwa na rafiki yake aliyeitwa Mwanangwa Marwa aliyekuwa akisoma Musoma.


Habari hizo zilimvutia, naye akatamani kwenda Shule ,lakini alitakiwa kupata baraka kutoka kwa wazazi wake. Awali ,Nyerere alimwendea mama yake ,Mugaya, na kumweleza amuombee ruhusa kwa Mzee Burito Nyerere ambaye hata aliposikia habari hizo hakuafiki kwa sababu alitaka mwanawe awe mtemi badala yake.


Alikuwa na hofu kuwa endapo Nyerere angekwenda mbali ya nyumbani kwake ,basi huenda angebadilishwa tabia na hangekuwa mtemi tena. Kwa nyakati hizo hakukuwa na Shule yoyote katika kijiji cha Butiama . Shule iliyokuwa karibu ilikuwa Musoma mjini umbali wa kilometa 42 kutoka Butiama.


Ingawa Mzee Burito Nyerere alikataa kumruhusu mwanae kwenda shuleni ,Nyerere hakukata tamaa ,alizidi kumhimiza mama yake azidi kumwombea ruhusa kutoka kwa Baba yake na hatimaye Nyerere aliruhusiwa kwenda shule. Nyerere alianza Shule akiwa na umri wa miaka 13, alianza masomo ya elimu ya Msingi mwaka 1935 katika Shule ya Mwisenge ,kilometa 42 kutoka Butiama. Kwa kuwa Butiama ilikuwa mbali na Musoma mjini, alipatiwa nafasi  ya kulala bwenini Musoma mjini.


Nyerere ambaye ni mtoto wa nne katika familia ya Mzee Burito yenye watoto wanane ,katika mtihani wake wa darasa la nne, alifaulu na kuchaguliwa kujiunga na shule ya Sekondari ya Tabora. Shule hiyo ilikuwa imejengwa maalum kwa watoto wa watemi ambapo alianza darasa la tano mwaka 1937 ambapo alichaguliwa kuwa kiongozi wa nyumba iliyoitwa Kifaru na aliongoza kwa kuchaguliwa mara mbili, kutokana na uongozi wake kuwa mzuri.


Alipokuwa shuleni  Tabora ,Nyerere alisikitishwa na kitendo cha viongozi wa mabweni kupendelewa kwa kupewa chakula kingi zaidi kuliko wanafunzi wengine. Alitaka wanafunzi wote watendewe haki sawa ambapo katika kupinga huko, jambo hilo lilikomeshwa mara moja. 


Alihitimu masomo ya Sekondari mwaka 1942 na alichaguliwa kuendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Makerere ,Uganda, na kuanza masomo yake januari ,1943 ambako alihitimu Shahada. Mwishoni mwa mwaka 1943 ,Nyerere alirudi nyumbani kuonana na jamaa zake ambapo alipata nafasi ya kubatizwa.


Alibatizwa na Padri Mathias Koenen Desemba 23, 1943 na baba yake wa ubatizo alikuwa Petro Masive. Nyerere alichagua jina la Julius kuwa la ubatizo. Wakati akiwa shuleni mara nyingi baada ya masomo alipendelea kusoma vitabu na magazeti chumbani kwake na wakati mwingine kwenye maktaba.


Akiwa Makerere wanafunzi wenzake walitambua mara moja ya kuwa Nyerere atakuwa mwanasiasa kutokana na kupendelea kujadili mambo ya siasa ,alipenda kuzungumza na wenzake kuhusu Ubaya wa kutawaliwa na wakoloni. Nyakati zile wanafunzi wengi wa Makerere walipendelea kucheza dansi, lakini Nyerere hakupenda kucheza alikuwa haendi kuangalia ,isipokuwa alipenda  Ngoma za jadi.


Pia hakupenda kunywa pombe hali iliyowafanya wanafunzi wenzake kufikiri kuwa Nyerere alitaka kuwa Padri, lakini hatimaye walishangaa kumwona akichaguliwa kuwa Mwalimu. Alirudi Tanzania mwaka 1945 ambapo alianza kuwa Mwalimu kwa kufundisha Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Maria, Tabora (sasa Mirambo).


Ingawa Nyerere alikuwa Mwalimu mwenye elimu ya juu, kamwe hakujivunia ,mara nyingi alipenda kuwa sawa na hata wanafunzi wake, Alizoea kucheza mpira pamoja nao wala haikuwa rahisi kumtambua alipokuwa kati ya wanafunzi wake, wakati mwingine walipokuwa michezoni na mvua ikawakuta huko. Mwalimu alichukua viatu vyake na kukimbia navyo akifuatana na wanafunzi wake.


Mwalimu Nyerere alikuwa hodari katika kazi yake hivyo akapendwa na wanafunzi wake ambao mara nyingi walimuiga mambo mengi ikiwa ni pamoja na jinsi alivyovaa nguo. Alivyotembea ,alivyochana nywele zake na hata alivyoongea. Licha ya kuwa Mwalimu Nyerere alipata elimu hadi Chuo Kikuu cha Makerere Uganda hakuridhika na elimu hiyo na alitamani kujiendeleza zaidi kielimu . Alipata nafasi ya kwenda chuo kikuu cha Edinburgh, Scotland mwaka 1949.


Katika Chuo hicho alichukua masomo ya juu ya sayansi ya jamii (MA) aliyoyamaliza mwaka 1952 na kufaulu . Alikuwa Mtanzania wa kwanza kupata shahada hiyo. Mwalimu Nyerere alirudi Tanzania mwaka 1952 na kufundisha katika shule ya Mtakatifu Francis ( sasa Pugu sekondari) umbali wa kilometa 20 kutoka jijini Dar es salaam. 


Mwalimu Nyerere alioa mwaka 1950, alioana na Mwalimu Maria Gabriel ,binti wa Gabriel Magige. Ndoa yao ilifungwa Januari 24 mwaka 1950 na Padri William Collins. Katika maisha yake ya ndoa Nyerere alifanikiwa kupata watoto saba, Andrew, Anna,Emil Magige, John,Makongoro, Madaraka ,na Rose. Nyerere alikuwa na zaidi ya wajukuu 22.


Katika kipindi hicho ndipo kilipoanzishwa chama cha TAA na wadau wenzake wanaotajwa kila siku wakiwemo ukoo wa kina Sykes,Mzee Tambaza, Mshume Kiate nk. Siku zile Tanganyika haikuwa na chama chochote cha kupigania Uhuru kwa wananchi, ingawa Nyerere hakuwa Dar es salaam lakini wenzake walimtambua haraka kuwa alikuwa mwanasiasa hodari,ndipo wakafikiria kumchagua kuwa Kiongozi wa TAA.


Oktoba 1953 alichaguliwa kuwa Rais wa chama hicho ,akaamua kujiuzulu ualimu baada ya kushawishiwa na kina Oscar Kambona, Mshume kiate, Mzee Tambaza, Dosa Aziz nk na wakoloni walimtaka achague moja kati ya ualimu au siasa. Mwaka 1954 Nyerere alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la kutunga sheria. Julai 7 mwaka 1954 kikazaliwa chama cha TANU, ambapo licha ya umri wake mdogo ,alichaguliwa tena kuwa Rais wa Chama hicho Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 32.


Aliongoza mapambano ya kusaka Uhuru yaliyokuwa na vikwazo vingi kutoka kwa wakoloni na baadhi ya wananchi ,lakini chini ya uongozi wake imara ,Tanganyika ilipata Uhuru kutoka kwa wakoloni wa kiingereza mwaka 1961 ambapo Mwalimu Nyerere aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza.


Tanganyika ilikuwa Jamhuri mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 40 ,Nyerere alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika. Aprili 26, 1964 nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwalimu Nyerere alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania.


Mwalimu ambaye alikuwa aliongoza kwa kufuata misingi ya Ujamaa na kujitegemea, aliifanya kazi ya Urais wa Tanzania kwa kipindi cha miaka 24 hadi alipoamua kung'atuka mwaka 1985 na kumwachia Rais wa awamu ya pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi. Mwl Nyerere ndiye muasisi wa Azimio la Arusha lililokuwa na lengo la kuweka uchumi mikononi mwa wananchi kutoka kwa mabepari na mali zilitaifishwa toka kwa mabepari na kuwa mali ya umma.


Mwaka 1974 ,chini ya uongozi wake ilipitishwa operesheni vijiji vya ujamaa vilivyokuwa na lengo la kuweka wananchi pamoja ili kupata huduma kwa urahisi. Mwaka 1977 akiwa Mwenyekiti wa chama cha TANU kwa upande wa Bara na Abdul Jumbe akiwa Mwenyekiti wa ASP upande wa visiwani ,walihusika kikamilifu kuviunganisha vyama hivyo na kuzaliwa CCM Februari 5, mwaka 1977.


Mwalimu Nyerere kwa mara nyingine alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa CCM wadhifa alioendelea nao hadi mwaka 1989 alipoamua kung'atuka na kumwachia Rais mstaafu wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi ,Mwalimu alitunukiwa shahada ya heshima ya udaktari kutoka Chuo cha Duquesne, Marekani na pia Vyuo vikuu vya Nigeria ,Liberia na Zimbabwe. Katika Miaka 77 ya maisha yake ,miaka 43 Nyerere alikuwa katikati ya siasa za Taifa letu. Nyerere kwa muda mrefu alikuwa ni Public opinion leader katika taifa letu hata baada ya kustaafu alikuwa akiombwa hata na wanaodai hawakukubaliana naye kifikra.





Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS