NA WILLIUM PAUL, SAME.
MAELFU ya Wananchi wa Tarafa ya Miamba katika Jimbo la Same mashariki wilayani Same mkoani Kilimanjaro wamejitokeza kushuhudia fainali ya mpira wa miguu ya aina yake ya Anne Kilango cup.
Fainali hiyo iliyozikutanisha miamba miwili ya soka ya Mpinji FC dhidi ya Mang'a FC ya kata ya Kirangare ambapo mchezo huo ulipigwa katika uwanja wa Miamba.
Mashindano hayo ambayo yamefadhiliwa na Mbunge wa Jimbo la Same mashariki, Anne Kilango Malecela huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa wilaya ya Same, Edward Mpogolo.
Mchezo huo ulioanza kwa kasi kubwa zilishuhudiwa dakika 90 zikimalizika kwa timu ya Mpinji FC kuibuka mshindi kwa kuifunga timu ya Mang'a FC goli 4 kwa bila.
Mshindi huyo aliweza kuibuka na zawadi ya jezi, mpira, medali, kombe pamoja na fedha taslim milioni moja huku mshindi wa pili Mang'a FC akiibuka na zawadi jezi, mpira, medali pamoja na fedha taslim laki nane.
Majira ya saa Saba mchana leo ilichezwa mechi ya kutafuta mshindi wa pili ambapo timu ya Vunta FC ilikipiga dhidi ya Goha FC kutoka kata ya Miamba.
Katika pambano hilo klabu ya Goha FC iliibuka mshindi wa tatu baada ya kuifunga vunta FC magoli matatu kwa moja na kuibuka na zawadi jezi, medali pamoja na fedha taslim laki sita.
Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi hizo, Mbunge wa Jimbo la Same mashariki, Anne Kilango Malecela alisema kuwa, lengo la kuanzisha mashindano hayo ambayo hushindanisha timu za tarafa yanalengo la kuwaunganisha vijana pamoja.
Alisema kuwa, michezo ni ajira na kuahidi kuhakikisha anaendeleza michezo katika Jimbo la Same mashariki.
"Rais Samia Suluhu Hasani anapenda michezo na yeye ndio ameagiza kila Mbunge kuhakikisha anaandaa michezo na mimi nimeamua kufanya ligi kitarafa ambapo leo tunafunga mashindano Tarafa ya Miamba na wiki ijayo tunaanza mashindano Tarafa ya Gonja na badae tunamalizia Tarafa ya Ndungu" alisema Mbunge Anne Kilango.
Naye Mkuu wa wilaya ya Same, Edward Mpogolo alisema kuwa, Mbunge wa Jimbo la Same mashariki, Anne Kilango Malecela amekuwa akifanya mambo mazuri na makubwa kwa ajili ya wananchi wake.
Mpogolo alisema kuwa, kuanzishwa kwa mashindano hayo na Mbunge huyo ni kuonyesha jinsi anavyowapenda na kuwathamini vijana.
Mkuu huyo wa wilaya alitumia nafasi hiyo kutoa salamu za Rais Samia Suluhu Hasani ambapo alisema Rais ameahidi kuhakikisha ujenzi wa kituo cha Afya Miamba kinakamilika pamoja na kukamilisha ujenzi wa barabara inayounganisha Tarafa ya Miamba.
"Rais anatambua wananchi wa Jimbo la Same mashariki wengi ni wakulima wa zao la Tangawizi hivyo atahakikisha bei ya zao inakuwa rafiki kwa wakulima ili kuwanufaisha" alisema Mpogolo.
Aidha alitumia nafasi hiyo kuagiza magari ya abiria yanayofanya safari zake kutoka Tarafa ya Miamba kwenda maeneo mbalimbali kuacha tabia ya kufanya safari zake majira ya kuanzia saa tisa za usiku na badala yake safari zote zianze saa kumi na mbili asubuhi ili kuufanya usafiri kuwa rafiki.
Awali akisoma taarifa ya mashindano hayo, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Same mashariki, Semu Mmamba alisema kuwa, mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 20 ambapo yaliendeshwa kwa mfumo wa makundi.
Mmamba alisema kuwa changamoto walizokumbana nazo ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya michezo kwa timu zilizoshiriki mashindano pamoja na miundombinu isiyo rafiki kwa michezo kama viwanja kuwa vidogo na kwenye miinuko.
Timu zote 20 zilizoshiriki mashindano hayo zilikabidhiwa jezi seti moja pamoja na mpira.
Mwisho...






















0 Comments