CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini kimeridhishwa na matumizi ya fedha za tozo kiasi cha shilingi milioni 760 ambazo zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kwenye sekta za elimu na afya.
Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka akizungumza akiwa na kamati ya siasa ya Wilaya baada ya kutembelea baadhi ya miradi hiyo iliyotekelezwa kwa fedha hizo amefurahishwa kwani miradi hiyo itaenda kutatua changamoto kwenye sekta hizo.
Nyamka akiwa kwenye mradi wa ujenzi wa madarasa ya shule ya Msingi Sofu alisema kuwa ujenzi wa madarasa hayo utasaidia kuondoa changamoto ya wanafunzi kusoma mbali.
Alisema kuwa shule hiyo ambayo imejenga baadhi ya madarasa na madawati ni mfano mzuri wa matumizi mazuri ya fedha hizo ambazo zimetokama na tozo .
"Haya ndiyo matokeo ya matunda ya tozo sababu kulikuwa na maswali juu ya fedha za tozo ambazo zimetumika kwenye sekta za elimu ambapo mashule yamejengwa bila kusahau afya kila mahali zimejengwa Zahanati na Hospitali,"alisema Nyamka.
Aidha alisema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan unapambana kuhakikisha huduma zinaboreka na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Kwa upande wake ofisa mipango wa Halmashauri ya Mji Kibaha Wambura Yamo alisema kuwa fedha hizo zinatekeleza miradi ya maendeleo kufuata ilani ya CCM.
Yamo alisema kuwa miradi hiyo wanaisimamia ili ikamilike kwa wakati iweze kutoa huduma kwa wananchi kama ilani inavyosema juu ya kuboresha utoaji huduma kwa jamii.
Ziara hiyo ya siku moja ilipitia miradi ya utoaji huduma za NHIF, CHF Zahanati ya Msangani, kukagua ujenzi wa madarasa na ununuzi madawati Sofu, maendeleo ya ujenzi wa soko jipya Tangini, mradi wa maji kwenye machinjio Pangani na kukagua ujenzi maabara kituo cha afya Mkoani Tumbi.
0 Comments