Na Frederick Siwale - Mdtv Media Makambako- Njombe.
MAAFISA Usafirishaji stendi ya mabasi Makambako Mkoani Njombe wametakiwa kuvaa mavazi yenye staha ,wakati wa kutoa huduma kwa abiria.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa maafisa usafirishaji abiria (UMAUA) stendi mpya ya mabasi Makambako Bw.Lucas Mlunza, kwenye mkutano wa dharula wa kushughulikia changamototo za maafisa usafirishaji.
Bw.Mlunza alisema stendi ya Mabasi Makambako ni lango kuu la kuingilia Mkoa wa Njombe ,hivyo Maafisa usafirishaji wanapaswa kuvaa sare na zenye unadhifu na siyo kuvaa mavazi ya kuendea kwenye makasino na nyumba za starehe.
"Kumbukeni kuwa stendi ya Makambako inapokea Wageni mbali mbali kutoka Mikoa jirani ya Iringa, Mbeya,Rukwa na Ruvuma, Lindi na Mtwara na hata Nchi jirani za Msumbiji, Malawi, DR.Congo, Zambia na Zimbambwe wanapita hapa, mnadhani wanapokuta maafisa mkiwa katika muonekano wa hovyo hovyo mnaitangazaje Makambako na Njombe ?" Alihoji Bw.Mlunza.
Aliongeza kusema kuwa Umoja wa Maafisa Usafirishaji abiria (UMAUA) kamwe hauwezi kufumbia macho vitendo vya uhalifu vikiwepo vya uvaaji nguo zinazo bana na kuonyesha maumbile ya ndani kwa akina dada na akina kaka kuvaa suruali bila mkanda " mlegezo"
Hivyo kuanzia sasa ni marufuku afisa usafirishaji kuvaa mavazi yasiyo na staha kwa muonekano wa Kitanzania na kuwataka watambulishwe kwa kuvaa sare na si vinginevyo.
Mmoja wa Wasafirishaji Majuto Kilimbe ,alitoa ushauri kwa Uongozi wa UMAUA kuhakikisha unasimamia katiba na kanuni za Umoja huo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa panapo tokea matatizo kama ugonjwa na msiba kati ya mwanafamilia ya UMAUA kuwepo na mshikamano na umoja wenye tija.
" Mwenyekiti naomba panapo tokea msiba iwepo kanuni inayolazimisha siku hiyo Wasafirishaji wote kusitisha kazi na kwenda kushiriki ,badala ya ilivyo hivi sasa wengine wanakwenda msibani wengine wanabakia kufanya kazi stendi." Alisema Bw.Majuto.
Hata hivyo Mwenyekiti Bw.Mlunza aliwataka maafisa usafirishaji kuondoa hofu kwani Uongozi umejipanga kushughulika na mapambano dhidi ya wavunja sheria za Nchi na kanuni za UMAUA na kwamba kamati ya nidhamu itashughulika na wote wavunjao taratibu na kanuni na vyombo vya ulinzi na usalama vitashirikishwa .
0 Comments