WAZAZI Wilayani Kibaha wametakiwa kuwalea watoto wao katika maadili mema na si kuwaachia walimu peke yao kwani mafanikio ya wanafunzi ni pande zote wazazi na walimu.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na mwenyekiti wa kikundi cha wanawake cha Pwani Generation Queens cha Mkuza Wilayani Kibaha Mkoani Pwani Berth Msimbe wakati mahafali ya 19 ya shule ya Msingi ya Jitegemee.
Msimbe alisema kuwa wazazi wasiwaachie watoto na kuona kama jukumu la kuwalea ni la walimu peke yao.
"Ili mtoto afanye vizuri kwenye masomo yake lazima pande zote mbili zihusike na siyo walimu peke yao,"alisema Msimbe.
Katika hatua nyingine kikundi hicho kilitoa fedha kiasi cha shilingi 300,000 kwa ajili ya kununulia mashine ya kudurufia karatasi (Photocopy Machine).
Kwa upande wa wanafunzi akisoma risala ya wahitimu Sadiq Rajabu alisema kuwa changamoto inayoikabili shule ni pamoja na ukosefu wa jengo la utawala, kisima cha maji na tenki la kuhifadhia maji.
Rajabu alisema kuwa changamoto nyingine ni upungufu wa matundu ya vyoo 31 na vyumba vya madarasa 11.
Naye Mwalimu mkuu wa shule hiyo Rahyana Mshana alisema kuwa anawashukuru wadau kwa kuisaidia shule yake na kuwataka wajitokeze kuisaidia ili iondokane na changamoto zinazoikabili.
Mshana alisema kuwa shule yake imekuwa na Maendeleo mazuri kitaaluma kwani miaka ya hivi karibuni imekuwa ikifaulisha kwa kiwango cha juu. Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 848 na katika michango ya ununuzi wa mashine ya kudurufu jumla kiasi cha shilingi 463,000 zilipatikana.
0 Comments