NA HAMIDA RAMADHAN,DODOMA
SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula Duniani (FAO) na Umoja wa Ulaya (EU),wamezindua mradi wa huduma za afya ya mimea mradi wenye thamani ya Euro Milioni 10.1 lengo likiwa ni kuhakikisha usalama wa Chakula na kuimarisha mfumo wa ukaguzi wa utoaji wa usafi wa Mazao yanayoingia na kutoka nchini.
Akizundua mradi huo jijini hapa Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde alisema uzinduzi huo umetokana na ukaguzi uliofanyika nchini mwaka 2017 katika mifumo maalumu ya udhibiti wa mimea na mazao yanayosafirishwa kwenda nchi za jumuiya ya Ulaya na ukaguzi huo kubaini mapungufu ya afya ya mimea.
“Niwashukuru EU na FAO kwa kufadhili mradi huu muhimu ni imani yetu kuwa malengo yaliyopangwa yatafikiwa na hivyo kuongeza upatikanaji wa masoko ya kimataifa na kuchochea uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja” alieleza.
Aidha Mavunde alitaja baadhi ya maeneo yaliyobainika kuwa na mapungufu hadi kupelekea kuanzishwa kwa mradi huo ni maarifa madogo kwa wakaguzi kuhusu matakwa ya usafi wa mazao hayo, kukosekana kwa mfumo kukusanya takwimu za visumbufu vya mimea, kukosekana kwa maabara zenye uwezo wa kufanya uchunguzi muhimu ili kuthibiti cheti cha usafi wa mimea.
“Kufuatia kubainika kwa mapungufu hayo na gharama za kufanya biashara ya mazao kuwa juu serikali ilichukua hatua kwa kuunganisha majukumu ya TPRI na ya afya ya mimea na viwatilifu TPHPA ambacho kimekuwa ni chombo kinachotambilika kimataifa” Alieleza Mavunde.
Hata hivyo alieleza kuwa kuja kwa mradi huu utawezesha kufikia malengo ya kuhakikisha ukuaji wa sekta ya kilimo hapa nchini kwa asilimia 10 na mauzo ya mazao ya kilimo yanaongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.2 za sasa hadi kufikia Dola bilioni 5 ifikapo mwaka 2030.
Alibainisha kuwa Wizara ya Kilimo itasimamia utaratibu na kuongeza utekelezaji wa mradi huo na kutaka kamati ya kusimamia mradi huo na kumtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo kuwasimamia wataalamu ili kazi zilizopangwa kwenye mradi zitekelezeke kwa wakati.
Awali Mwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Obadia Nyagilo alisema mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha mika mitatu na nusu kwa kiasi cha Euro milioni 10.1 kwa ushirikiano ambapo Jumuiya ya umoja wa Ulaya itatoa Euro milioni 9.5, FAO itatoa Euro 350’000 na Tanzania itatoa EURO 250,000.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya mimea na Uthibiti wa Viuatilifu Tanzania (TPHPA) ,Dk.Efrem Njau alisema sekta ya kilimo ni muhimu sana ambapo imeajiri zaidi ya asilimia 67 ya watanzania na kuchangia takribani asilimia 29 ya pato la taifa.
Dkt, Njau alitaja baadhi ya majukumu yanayofanywa na mamlakae hiyo kuwa ni kusimamia na kuratibu tasnia nzima ya viuatilifu, kudhibiti ubora, uagizaji, usambazaji na kuchagiza matumizi sahihi na usalama wa viuatilifu, kufanya uchambuzi wa athari ya visumbufu.
"Matokeo tarajiwa ya mradi huo ni kuziongezea uwezo maabara za mamlaka kujenga, kukarabati na kuweka vifaa katika maabara za Mamlaka, kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa visumbufu na masalia ya viuatilifu katika mnyroro wa thamani ya uzalishaji wa mazao hususa ni yale mbogamboga na matunda” alisema.
Aliongeza kuwa mradi huo utakuwa na kamati ambayo itaundwa na itawajibika kukutana na mara mbili kwa mwaka kupitia na kuhakikisha malengo ya mradi yanakwenda kama yalivyopangwa.
Nae Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (FAO),Nyebenyi Tipo alisema mradi huo umelenga kuhakikisha usalama wa Chakula hasa kwa mazao yanayovuka mipaka kwa kuhakikisha yanakuwa na ubora na kuhakikisha usalama wa chakula na FAO watatoa ushirikiano kuhakikisha mradi huo unatekelezeka na unaleta tija kwa kukuza sekta ya kilimo na mazao nchini na nje ya nchi.
Mwisho
0 Comments