Na THABIT MADAI, MATUKIO DAIMA APP, ZANZIBAR
KUFUATIA Kuenea kwa Video kwenye Mitandao ya Kijamii ikiwaonesha Wanaume wakichumbiana hadharani, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadid amekemea kitendo hicho na kuwaahidi kuwachukulia hatua za Kisheria.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kitendi hicho ni kinyume na Sheria na Utaratibu wa Nchi hivyo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inalaani kitendo hicho.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo huko Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kitendo kilicho fanywa na vijana hao ambao ni raia wa kifaransa ni kinyume na taratibu za Nchi hivyo Serikali itaendelea na hatua mbalimbali za Uchunguzi na kuwachukulia hatua stahiki.
“Tumeona na Tumepokea taarifa mbalimbali kuhusu hawa Vijana Raia wa Kifaransa wakifanya vitendo ambavyo ni kinyume na utaratibu wa Nchi, Dini na utamaduni wetu wa kizanzibar hivyo sisi Serikali tuwawachukulia hatua kwa Mujibu wa Sheria,” amesema.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Wananchi kuwa Watulivu huku Serikali ikiendelea na hatua mbalimbali za kisheria.
“Niwaombe Wananchi kuwa watulivu katika Kipindi hichi wakisubiri Serikali iendelee na hatua mbalimbali za kuwachukulia hatua Vijana hao,” ameeleza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini inaungana na Ofisi ya Mufta Zanzibar pamoja na Kamisheni ya Utalii Zanzibar kulaani kitendo hicho kilichofanywa na Wageni hao mnamo tarehe 20 Septamba mwaka huu katika fukwe za bahari ndani ya Mkoa wa Kusini Unguja.
0 Comments