NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Daniel Chongolo amemuagiza Mkuu wa wilaya ya Moshi kupitia wataalam wa Manispaa kuhakikisha ndani ya wiki moja wafanye tathimini ya gharama pamoja na michoro ya ujenzi wa soko la Manyema Manispaa ya Moshi.
Hatua hiyo imefikia baada ya wakinamama waliokuwa wakifanya biashara katika soko hilo kwa kuuza samaki wabichi kumlilia Katibu Mkuu huyo huku wakiwa wameshika majana na kumpigia magoti kuondolewa mwaka huu na kutakiwa kuhamia soko la Pasua.
Katibu Mkuu Chongolo alisema kuwa, wataalam wanatakiwa kufanya tathimini ya ilo eneo na kuona kama linafaa kwa ajili ya ujenzi wa soko na kama litafaa wachore na mchoro na kuiwasilisha kwake ili aweze kufanya msukumo kupata fedha za ujenzi wa soko hilo.
"Mkuu wa wilaya nakuachia hili jambo simamia ndani ya wiki moja wataalam wafanye tathimini ya ilo eneo na kufanya tathimini pamoja na michoro ndani ya wiki moja mniletee ili tuweze kufanya msukumo kupata fedha za ujenzi wa soko hilo" alisema Katibu Mkuu Chongolo.
Awali akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa wilaya ya Moshi, Abbas Kayanda alisema kuwa, eneo hilo sio rafiki kwa kufanyia biashara kwa sasa kwani hakuna miundombinu rafiki kiafya hali iliyokuwa imepelekea kupanga bidhaa zao chini.
"Eneo la Manyema linafaa kwa kufanyia biashara ya soko endapo likijengwa soko la kisasa kwani linafaa kwa biashara lakini kwa sasa halifai mpaka miundombinu itakapotengenezwa" alisema Kayanda.
Alisema kuwa, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ilitenga milioni 250 kwa ajili ya ukarabati wa soko la Pasua na ujenzi wa vyoo katika masoko mengine ili wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara zao katika soko la Manyema kuhamia huko.
Ikumbukwe kuwa toka kuondolewa kwa wafanyabiashara wa samaki katika soko hilo la Manyema na kutakiwa kuhamia katika soko la Pasua walikataa na kuamua kuhamia katika soko la Mailisita lililopo Halmashauri ya Hai.
Mwisho...
0 Comments