Iwapo Raila Odinga atawasilisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi, itasikilizwa na majaji wa Mahakama ya Juu zaidi
Zoezi la kupiga kura nchini Kenya lilikamilika baada ya raia kupata fursa ya kuchagua viongozi wao wa ngazi mbali mbali na matokeo kutangazwa na mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Wafula Chebukati.
Kati ya wagombea wanne waliokuwa wanapigania kuchukua nafasi ya Uhuru Kenyatta, Wafula Chebukati alimtangaza William Ruto kuwa ndiye mshindi wa Urais katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, hali ilibadilika pale mpinzani mkuu Raila Odinga ambaye pia ni kinara wa Muungano wa Azimio la Umoja kutangaza kuwa hakubaliani na matokeo ya urais.Wakati anazungumza, Raila Odinga alisema kwamba hakubaliani na matokeo hayo kwasababu mwenyekiti wa tume hiyo alikiuka katiba kabla ya kumtangaza mshindi.
Alisema kwamba makamishna wa tume hiyo hawakukubaliana kuhusu hesabu ya mwisho ya matokeo hayo yaliompatia ushindi William Ruto.
''Takwimu zilizotangazwa na Chebukati ni batili, kwa maoni yetu hakuna mshindi kisheria aliyetangazwa kihalali wala rais mteule''.
Na kauli hiyo, inaonesha kuwa moja ya machaguo aliyo nayo Raila Odinga katika kukabiliana na hilo, nikuwasilisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi ya urais katika Mahakama ya Juu Zaidi.
Ombi hilo litakapowasilishwa, litasikilizwa na jopo la majaji saba.
Majaji hao ni Jaji Mkuu Martha Koome, Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, William Ouko, Mohamed Ibrahim, Smokin Wanjala, Njoki Ndung’u na Isaac Lenaola.
Jaji Mkuu wa Kenya Martha Koome
Jaji Martha Koome ni wakili na mtetezi wa haki za kibinadamu.
Aliweka historia Mei 21, 2021 kwa kuwa jaji mkuu wa kwanza mwanamke nchini humo.
Bi Martha aliidhinishwa rasmi kuwa wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya mwaka 1986 na baada ya hapo akafungua kampuni yake ya uwakili ambayo aliisimamia hadi 2003.
Pia kuna wakati alihudumu kama mwanachama wa baraza la Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK).
Mnamo mwaka 2012, alipandishwa hadi Mahakama ya Rufaa na Septemba mwaka huo huo, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mahakimu na Majaji wa Kenya.
Hizi, miongoni mwa juhudi zake nyingine kwa ajili ya ustawi wa watoto, alipongezwa kama mshindi wa pili wa Tuzo za Umoja wa Mataifa nchini Kenya 2020.
Koome ni mtetezi anayesifika wa haki za binadamu, akizingatia zaidi haki za wanawake na watoto.
Zaidi ya hayo, Martha Koome ni mtaalam aliyebobea katika masuala ya sheria ya familia, eneo ambalo amekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za mali katika ndoa, hasa kwa wanawake.chanzo :BBC
0 Comments