NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Ziara ya Mbunge wa Jimbo la Moshi vijijini Profesa Patrick Alois Ndakidemi imehitimishwa kwa kuzifikia Kata za Oldmoshi Mashariki, Oldmoshi Magharibi na Uru Mashariki.
Katika ziara yake, alikukutana na viongozi wa Chama Kata na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara ambapo aliongozana na Katibu wa Umoja wa Wazazi Wilaya ya Moshi Vijijini Andrea Mwandu.
Katika ziara hiyo, Ndakidemi alipata nafasi ya kukutana na Kamati za Siasa za Kata na kuwapongeza kwa kuchaguliwa kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano.
Katika ziara yake, akiwa Kata ya Oldmoshi Mashariki, Mbunge alitembelea mradi wa ujenzi wa choo cha Shule ya Msingi Matemboni kilichofadhiliwa na mfuko wa jimbo.
Alielezwa kuwa wadau wa maendeleo wanasaidia kukamilisha ujenzi huo, vilevile, akiwa Uru Mashariki, alikagua ujenzi wa barabara ya Mamboleo - Materuni inayejengwa kwa kiwango cha lami.
Wakimkaribisha Mbunge kuongea na wananchi kwa nyakati tofauti, Madiwani wa Kata za Oldmoshi Mashariki na Uru Mashariki, Jane Mandara na Samueli Materu walieleza wananchi mafanikio makubwa yaliyotekelezwa na Serikali katika Kata hizo.
Mafanikio kwa upande wa Oldmoshi Mashariki ni pamoja na ujenzi unaoendelea wa barabara ya Kiboriloni - Tsuduni - Kidia kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi bilioni 4.6 huku Uru Mashariki wanajivunia kukamilika kwa daraja la Rau ambalo limegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja.
Akiongea na wananchi kwa nyakati tofauti katika ofisi za huko Oldmoshi Mashariki na Uru Mashariki, Ndakidemi aliwahamasisha wananchi washiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa kwani inasaidia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa mipango ya Maendeleo ya watu katika ngazi husika.
Akiwa Oldmoshi Mashariki na Uru Mashariki, Mbunge aliwaambia wananchi kwamba Serikali imetenga fedha za kutosha na elimu itakuwa bure bila malipo kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita katika shule za Serikali.
Aliwaambia, azma ya serikali ni kuhakikisha inawakwamua watoto wote waweze kujipatia elimu bure ambapo taarifa hiyo iliamsha shangwe na furaha katika mkutano.
Katika mikutano yote iliyofanyika katika Kata za Oldmoshi Mashariki na Uru Mashariki, Prof. NDAKIDEMI aliwaambia wananchi kuwa bunge la bajeti limeongeza fedha za Wizara ya Kilimo kutoka bilioni 294 hadi bilioni 954.
Alisema, serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele kuendeleza sekta ya kilimo ambayo imeajiri idadi kubwa ya Watanzania hivyo ongezeko hilo la bajeti litasaidia kuboresha huduma za ugani, kusaidia uzalishaji wa mbegu bora za mazao mbalimbali, ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, na ruzuku ya mbolea na kila Afisa ugani ameshapewa pikipiki ili aweze kuwafikia wakulima kirahisi.
Aliwashauri wakulima wa kahawa kuchangamkia fursa ya kupatiwa miche ya kahawa na serikali kwani imejipanga kuzalisha miche ya kahawa milioni 20 ambayo watagawa bure kwa wakulima.
"Niwaombe wakulima wa kahawa kutoka jimbo la Moshi Vijijini mjipange mapema ili serikali itakapogawa miche tuwe tumeandaa mazingira ya kuipanda miche hiyo chotara kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Lyamungo huzaa kwa kiwango kikubwa na huweza kukabiliana na magonjwa" alisema Prof. Ndakidemi.
Mbunge aliwaeleza kuwa serikali imetenga shilingi bilioni 150 kwa ajili ya ruzuku ya mbolea ambapo itasaidia kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya bei za mbolea kwenye soko la dunia, na hivyo kuwawezesha wakulima kuzinunua kwa bei nafuu.
Mbunge alisema kwamba mfuko wa mbolea aina ya Urea utanunuliwa kwa shilingi elfu 70,000 badala ya 140,000 ambayo ni bei ya sasa madukani huku pia serikali itawasaidia wananchi wanaolima maparachichi kupata miche bora kwa bei ndogo.
Wakitoa kero zao, wananchi wa Kata za Oldmoshi Mashariki na Uru Mashariki walieleza kuwa ubovu wa barabara ni tatizo linalowatesa sana hasa wakati wa kipindi cha mvua.
"Barabara ya Mahoma na ile ya Mamboleo - Kishumundu - Materuni ni mbovu sana, na mkandarasi aliyekuwa anatengezeza amezidisha tatizo la utelezi kwani hajaweka Changarawe, na barabara ya Mamboleo - Kishumundu - Materuni ndiyo njia inayopeleka watalii katika eneo la Materuni Waterfalls na kuingizia nchi pesa za kigeni" walisema.
Waliiomba Serikali itekeleze ahadi ya kuijenga kwa kiwango cha lami kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi huku barabara nyingine iliyolalamikiwa ni ile ya kwenda kwenye Kituo cha Afya Kyaseni.
Kwenye Kata zote mbili alizotembelea, Mbunge alipokea changamoto za wananchi kutokupata maji safi na salama.
Katika kata ya Uru Mashariki, wananchi walilalamika kukosa maji katika baadhi ya vijiji huku wakidai kuwa wao wanaishi karibu na vyanzo vya misitu ya mlima Kilimanjaro na maji yapo hayahitaji hata umeme kusukuna kuwafikia.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Uru Mashariki Sisti Mashoro alimwomba Mbunge awasilishe kero ya Kituo cha Afya Kyaseni ya kutokuwa na gari la kubeba wagonjwa.
Changamoto nyingine iliyolalamikiwa na wananchi ni ukosefu wa maji ya kumwagilia kutokana na uharibifu wa mifereji ya asili.
Wananchi walisema kuwa miaka ya nyuma mifereji ya umwagiliaji ya asili ilikuwa ikiwapatia maji ya kumwagilia kahawa na mazao mengine kama ndizi lakini hivi sasa hali sii nzuri na kuiomba serikali iwasaidie kuboresha mifereji ya asili ya umwagiliaji ambayo kwa sasa ina hali mbaya ili iwasaidie wawe na kilimo cha tija.
Mbunge akiwa katika Kata ta Oldmoshi Mashariki, Diwani wa Kata hiyo, Jane Mandara alieleza umuhimu wa kuwa na hosteli ya wasichana katika shule ya sekondarim ya Meli.
Mkazi wa Oldmoshi Mashariki ajulikanaye kwa jina la Julius Mshiu alilalamika kwamba wazee wengi wasio na uwezo wametelekezwa bila huduma za chakula na dawa za matibabu na kuwafanya waishi kwa shida huko vijijini na kuiomba serikali itafute namna ya kuwasaidia.
Akichangia katika mkutano wa Mbunge, mkazi wa Tsuduni Aika Lyatuu ameiomba serikali ije na mikakati ya kuwasaidia wananchi kuwazuia Tumbili ambao wamekuwa kikwazo kwa wananchi kufanya shughuli za kilimo kwani Wanyama hawa ni waharibifu na wanasababisha umaskini kwa wakulima.
Akijibu kero za wananchi kwa nyakati tofauti, Prof. Ndakidemi aliipongeza Serikali kwa kuwapatia pesa za kutekeleza miradi ya maendeleo katika Kata za Oldmoshi Mashariki na Uru Mashariki fedha ambazo zimeelekezwa katika miradi ya barabara, maji, umeme, elimu na afya.
Prof. Ndakidemi aliwataka wajenzi wa barabara za Moshi vijijini wanaosimamiwa na TARURA kuwa makini na kuhakikisha viwango tarajiwa vinazingatiwa ili kuitumia fedha iliyotolewa na serikali kwa tija.
Aliahidi kufikisha changamoto zote za ubovu wa barabara kwa meneja wa TARURA Moshi na zile za mifereji ya asili kwa mhandisi wa umwagiliaji wa Kanda ya Kaskazini.
Mbunge aliwaomba wananchi washiriki kikamilifu kwa hali na mali na kuisaidia serikali kutekeleza miradi ya kutengeneza barabara, mifereji ya asili, vyoo vya shule na kukarabati madarasa yaliyochakaa.
Kuhusu kero ya maji, alisema atajitahidi ili wananchi wa Kata za Oldmoshi Mashariki na Uru Mashariki wapate huduma ya maji safi na salama katika sehemu ambazo maji ya bomba hayajafika na kuahidi kuwasiliana na mamlaka ya maji MUWSA na kufikisha kero zao.
Kwa upande wa ujenzi wa bweni katika shule ya Sekondari ya Meli, Mbunge Ndakidemi ameahidi kushirikiana na wananchi katika ujenzi huo huku kero ya gari la wagonjwa Kyaseni atawasilishwa TAMISEMI.
Kuhusu huduma kwa wazee, Ndakidemi ameitaka jamii yote kwa ujumla wabebe jukumu la kuwatunza wazee kwa sababu nguvu zao za kutafuta kipato zimepungua na kuviomba vituo vya afya, zahanati na hospitali zitoe huduma kwa wazee bila kuwanyanyapaa.
Akiongea kwa nyakati tofauti, Katibu wa Umoja wa Wazazi CCM Wilaya ya Moshi vijijini, Andrea Mwandu aliipongeza Serikali kwa utekelezaji makini wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020.
Alisema kwamba CCM itaendelea kuisimamia serikali ili iendelee kuwekeza katika maendelea ya wananchi na taifa lote kwa ujumla.
Baada ya kujibu kero za wananchi Wenyekiti wa CCM Kata za Oldmoshi Mashariki na Uru Mashariki walifunga vikao kwa kumshukuru Mbunge kwa kuwatembelea, na Wanachi kwa kuja kumsikiliza Mbunge wao.
Mwisho.
0 Comments