NA HAMIDA RAMADHAN DODOMA
MKURUGENZI Mkuu Mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) Adam Fimbo amesema jumla ya kiasi na thamani ya bidhaa za dawa na vifaa tiba visivyofaa kwa matumizi ya binadamu zilizoteketezwa imeongezeka kutoka tani 14,704.80 zenye thamani ya TZS 8.5 bilioni zilizoteketezwa mwaka 2020/21 na kufikia jumla ya tani 35,547.47 zenye thamani ya takribani TZS 35.53 bilioni zilizoteketezwa mwaka 2021/2022.
Akiongea na waandishi wa habari Mkurugenzi huyo Wakati akieleza utekekezaji wa shughuli za mamlaka hiyo kwa Kipindi Cha mwaka wa fedha 2022/2023 Alisema Bidhaa hizo zinajumuisha bidhaa zilizotolewa taarifa na zile zilizokamatwa katika kaguzi mbalimbali.
Alisema kuongezeka kwa bidhaa zilizoteketezwa kunatokana na kuimarisha ukaguzi na elimu kwa umma inayosaidia wateja kutoa taarifa juu ya bidhaa zisizofaa kwa matumizi.
"Kazi kubwa ambazo tumefanya lengo letu kubwa nikudhibiti bidhaa na mfumo wa ufuatiliaji wa madhara," Alisema Mkurugenzi Fimbo
TUMBAKU
Alisema kuhusu udhibiti wa bidhaa za tumbaku Mamlaka iliandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2021-26) wa Kitaifa wa Kupambana na Tumbaku pamoja na Mpango Kazi wa Miaka Mitano wa Udhibiti wa Tumbaku ambao umeanza kutekelezwa.
"Tumeweka tayari mfumo wa udhibiti wa bidhaa hizi na hadi sasa tumekwishatambua bidhaa zote za tumbaku zilizoko kwenye soko ambapo idadi yake hadi sasa ni bidhaa 51,"
Aliendelea kueleza kuwa " Mamlaka imeanzisha maabara ya upimaji wa bidhaa za tumbaku kwenye jengo lake lililoko hapa Dodoma," Alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha alisema ufuatiliaji wa madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa Mamlaka imeweka mifumo madhubuti ya ufuatiliaji wa madhara yatokanayo na matumizi ya dawa, chanjo na vifaa tiba (kitaalam vigilance system) ili kuweza kubaini, kutathmini na kuzuia madhara yasiyovumilika yasitokee kwa wananchi.
Aidha, ili kuimarisha upatikanaji wa taarifa hizo, TMDA imeanzisha mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama ADR Reporting Tool wa utoaji wa taarifa za madhara yatokanayo na matumizi ya dawa kwa kutumia simu za mkononi au kompyuta na kwa njia ya kutuma ujumbe mfupi kwenye simu.
Kupitia mfumo huu TMDA imepokea jumla ya taarifa 4,898 katika kipindi husika na hadi sasa kuna jumla ya taarifa 31,666 kwenye Mfumo wa Taarifa unaosimamiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ujulikanao kama Vigibase.
0 Comments