Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imeaswa kuanzisha programu maalumu ya kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wafanyabiashara, ambayo itawasaidia kujiinua kiuchumi kupitia mikopo inayotolewa na benki hiyo.
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa Wilaya ya Bukoba Moses Machali, wakati akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge, katika uzinduzi rasmi wa TCB tawi la Bukoba.
Machali amesema kuwa baadhi ya wananchi wanashindwa kunufaika na huduma zinazotolewa na benki hiyo, kutokana na kutokuwa na ufahamu wa namna gani wanaweza kuboresha biashara zao kupitia mikopo.
"Kulingana na soko lilivyo katika hali ya uchumi wa sasa hivi, na kwa sababu wilaya hii ya Bukoba ina wananchi na wafanyabiashara wengi ambao wanatamani kujikwamua kiuchumi, hivyo hii ni fursa nzuri kwao na kwa benki kuweza kuandaa mafunzo ya ujasiriamali, ili wananchi waweze kunufaika na fursa mbalimbali " amesema Machali.
Kwa upande wake afisa mtendaji mkuu wa TCB hapa nchini Sabasaba Moshingi amesema kuwa shilingi bilioni 720 zimetolewa kama mikopo kwa watu mbalimbali kwa ajili ya kuwawezesha kukua kiuchumi.
Amesema kuwa katika kiasi hicho cha fedha kilichotolewa mkopo Kwa wananchi, shilingi bilioni 9.3 kimekopeshwa kwa wananchi wa Kagera.
Nao baadhi ya wafanyabiashara akiwamo Remigius Patrick, wakizungumza wakati wa uzinduzi huo wameitaka benki hiyo kuona umuhimu wa kuanzisha tawi katika eneo la Mutukula ambako ni mpakani mwa Tanzania na Uganda, kutokana na eneo hilo kuonekana kukua kwa kasi.
0 Comments