Header Ads Widget

SERIKALI YAAGIZA UKAGUZI MAKAO YA WATOTO DAR

 


Afisa Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Hassan Rungwa (mwenye suti) akizindua mradi mpya wa kuimarisha malezi mbadala chini ya Shirika la SOS Village.

NA ARODIA PETER  MATUKIODAIMAAPP,Dar es Salaam

Serikali Mkoa wa Dar es Salaam imeziagiza halmashauri zote  jijini humo kufanyia ukaguzi vituo vya makao ya watoto waliokuwa kwenye mazingira magumu ili yakidhi viwango vya kisheria.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Hassan Rugwa alitoa agizo hilo jana Julai 21,2022 wakati akizindua mradi mpya wa kuimarisha malezi mbadala kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu katika jiji hilo chini ya Shirika la SOS Village. 


Rungwa alisema Mkoa wa Dar es Salaam una vituo 59 vya kulelea watoto lakini 27 kati yake havijapata usajili kwakuwa havijakidhi vigezo vya kisheria na hivyo kuwa hatarini kufungiwa.


Hata hivyo alisema serikali haina mpango wa kufungia vituo kwakuwa vinafanyakazi nzuri ambayo inaisaidia serikali, lakini ni vema wahusika wajitahidi kukamilisha vigezo vinavyohitajika.


"Naziagiza halmashauri zote za Dar es Salaam  kuhakikisha makao yote ya watoto kwenye maeneo yao  yanakaguliwa ili yakidhi vigezo


"...Serikali haina wala isingependa kuvifungia kwakuwa vinafanyakazi nzuri, hivyo tuwasaidie kufikia vigezo na viwango vinavyotakiwa" alisema Rungwa.


Katika hatua nyingine, Katibu Twala huyo aliisifu SOS kwa kubuni mradi huo ambao unafanywa kwa ushirikiano na nchi za Tanzania, Kenya na Rwanda.


Alisema mradi huo pia unahusisha kikosi maalum kitakachohusika na ulinzi dhidi ya  usafirishaji wa binadamu ambao unaweza kuathiri nchi zote tatu.


"Nichukue nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza SOS Village kwa kutambulisha mradi huu, serikali tunatambua mchango mkubwa wa shirika hili, tunatambua umuhimu na uzito wa miradi mnayoisimamia, tuko tayari kutoa ushirikiano kwa nguvu zote"alisema Rungwa.


Akizungumzia mradi huo, Mratibu Mkuu wa Malezi mbadala wa SOS Village, Onesmo Itozya alisema mradi huo wa kuboresha malezi mbadala kwa jamii unalenga mambo matatu ambayo aliyataja kuwa ni pamoja na kuimarisha mifumo kwa kuwajengea uwezo walezi wa watoto walio kwenye mazingira magumu na hatarishi huku pia wakiimarisha uchechemuzi wa mifumo yote ya kisheria.


Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Nyamara Elisha alisema sheria inawataka wamiliki wa makao ya watoto kuwalea bila kuwafanyia ukatili watoto. 


Kuhusu sifa zinazohitajika kwa makao ya watoto waliotoka kwenye mazingira nagumu, Elisha alizitaja kuwa ni pamoja na kuwa na majengo ya kudumu, kuwa na walezi wenye sifa ya ngazi ya cheti cha ustawi wa jamii.


"Sifa nyingine ni jengo hilo la makao lazima liwe na uzio ili watoto wadogo kwa ujumla wawe kwenye ulinzi ili hata wanaotambaa wasiwezi kugongwa na vyombo vya moto.


"Pamoja na hayo lazima makao hayo yawe na eneo la michezo na vyoo vizuri na bora" alisisitiza Elisha.


Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Ubungo, Zainabu Masilanga alisema wilaya hiyo ni muhanga wa watoto wa mitaani kutokana na uwepo wa Standi Kuu ya Mabasi ya Magufuli.

 

Alisema standi hiyo inazalisha watoto wa mitaani waotoka mikoani kwa wastani wa watoto wawili hadi wanne kwa wiki.

Ili kukabiliana na wimbi hilo kubwa  wamefungua kituo maalum cha maafisa ustawi wa jamii kwenye standi hiyo ili kuwakusanya watoto wote wanaotoroka makwao kuja  jijini Dar es Salaam kwa  lengo la kutafuta kazi.

"Mpango huo wa kufungua ofisi ya Ustawi pale Standi ya Magufuli imezaa matunda kwani tumefanikiwa kuwakusanya watoto na kuwapa elimu na mifano mbalimbali ambapo baadhi yao huomba kurudi makwao kwa hiari.

"Na hii nikwa sababu Ubungo ni lango la jiji, kwa ujumla tunajitahidi lakini kwa Wilaya nzima ya Ubungo, eneo la Kijaji Interchange ni eneo korofi kwani lina watoto wengi wa mtaani" alisema.


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI