**********
Na Fatma Ally Matukio Daima APP Dar es Salaam
Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (RUCU) kilichobobea katika kutoa kozi mbalimbali ikiwemo Afya, Sheria Komputa Sayansi, Ualimu, Biashara kuanzia ngazi ya astashaha, stashahada na shahada zinazotambulika na TCU kimewataka wazazi na walezi kuwawapeleka watoto wao katika chuo Ili kuweza kujipatia elimu na ujuzi ambao utapelekea kuweza kujiajiri wenyewe mara baada ya kuhitimu masomo yao.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa kozi za Shahada na zisizo za shahada kutoka chuo hicho, Dr Willy Migodela wakati alipokua akizungumza na Mtandao wa Matukio Daima kwenye banda lao katika maonyesho ya 17 ya vyuo vikuu yanayoendelea katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa, mbali na mafunzo yanayotolewa katika chuo pia wefanikiwa katika masuala ya tafiti ambapo vijana wao wameweza kutengeneza dawa za kikohozi na fangasi kwa kutumia miti ya asili lakini bado zinafanyiwa mazoezi na zinafanya vizuri, hivyo zitafikishwa katika mamlaka husika mara baada ya kukamilika.
"Vijana hawa watakapotoka chuoni sio lazima waajiriwe kwani wataweza kujiajiri wenyewe kutokana na maarifa makubwa walioyapata, huu ndio utofauti mkubwa uliyopo kati yetu na vyuo vyengine, wanaweza kuwaajiriwa hata katika Taasisi za masula ya tafiti"amesema Dr Willy.
Hata hivyo,amesema katika kozi za sayansi ya kompyuta na software engineering tayari chuo cha RUCU wameandaa project mbalimbali ikiwemo teknolojia ya kufunga sensa maalum katika magari ya mizigo itakayozuia agari hayo kubeba mizigo inayozidi uzito wa kiwango cha gari kubeba.
"Kwa teknolojia hii waliyokuja nayo vijana wa chuo chetu ni kwamba gari lolote la mizigo lililopakia mzigo ambao umezidi uzito, gari litagoma kuwaka na litatoa alarm na meseji kuwa gari mzigo umezidi na itamlazimu mwenye gari kupunguza uzito wa mzigo ambapo gari itawaka na kuendelea na safari jambo litakalopunguza uharibifu wa barabara na mizani mbalimbali za barabarani na hichi ni moja kati ya vifaa vilivyobuniwa na vijana wetu"aliongeza Dkt Migodela.
Ameongeza kuwa, vijana wa chuo hicho pia wametengeneza mashine maalum ya juisi ambayo itawawezesha wateja kupimiwa juisi kulingana na kiwango cha fedha ambacho watakiweka katika mashine hiyo sambamba na kubuni kifaa maalum cha kuzuia mbu ndani ya nyumba ambayo itasaidia kupunguza magonjwa hasa malaria.
Amesema kuwa, Chuo hicho kilichopo mkoani iringa kina mazingira mazuri sana ya kujisomea na tulivu muda wote, hivyo amewataka wazazi walezi na wanafunzi kuweza kufika katika Banda lao kuweza kupata ufafanuzi zaidi ya kozi wanazozitoa.
Maonyesho ya 17 ya elimu ya juu sayansi na teknolojia yameanza Julai 18,2022 katika Viwanja vya mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam hadi Julai 23,2022 na yanatarajiwa kufunguliwa rasmi leo na waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kasim Majaliwa Mbunge.







0 Comments