Header Ads Widget

SUA: PPP NDIYO NJIA YA KUFANYA KILIMO KUWA INJINI YA UCHUMI

Naibu Makamu mkuu wa chuo Kikuu SUA Prof Amandus Muhairwa

Na Matukio Daima Media,Morogoro

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimesema mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) una nafasi kubwa ya kuibadilisha sekta ya kilimo na kuifanya kuwa mhimili wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania, kikisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za elimu ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya Taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Amandus Muhairwa, wakati wa Mhadhara wa Wazi ulioandaliwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), akisema chuo hicho kinaunga mkono juhudi za kituo hicho za kujenga uelewa kuhusu nafasi ya PPP katika maendeleo ya sekta mbalimbali.

Prof. Muhairwa amesema SUA imefarijika kuwa sehemu ya taasisi zinazoshirikishwa katika mjadala wa ubia kwa kuwa kilimo ndicho uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania na maendeleo yake yanategemea uwekezaji, utafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia.

Amesema hakuna viwanda imara bila kilimo chenye tija, hivyo kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za utafiti kutasaidia kuongeza uzalishaji, kuinua thamani ya mazao, kuongeza ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Prof. Muhairwa amesema SUA ipo tayari kushirikiana na PPPC katika tafiti na ubunifu utakaosaidia kuvutia uwekezaji na kuifanya sekta ya kilimo kufikia malengo yaliyowekwa ifikapo mwaka 2030.

Awali akitoa mhadhara huo, Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila, amesema Tanzania inaweza kufanikisha malengo hayo kwa kutumia kikamilifu mfumo wa PPP, akieleza kuwa mataifa yaliyopiga hatua kiuchumi, ikiwamo China, yalitumia ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kuharakisha maendeleo.


Kafulila amesema uchumi wa Tanzania unahitaji mbinu mpya za kufadhili miradi ya maendeleo badala ya kutegemea mikopo pekee, huku PPP ikiwa moja ya njia zinazoweza kuongeza uwekezaji na ufanisi bila kuathiri umiliki wa Serikali.


Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutofautisha PPP na ubinafsishaji, akieleza kuwa ubia unahusu ushirikiano katika utekelezaji au uendeshaji wa miradi huku mali ikiendelea kubaki chini ya umiliki wa umma.


Katika kufafanua hilo, Kafulila ametolea mfano Reli ya Kisasa (SGR), akisema Serikali inaweza kushirikiana na kampuni yenye uzoefu katika uendeshaji wa reli hiyo ili kuongeza tija na mapato bila kuuza au kuhamisha umiliki wake.


Aidha, amesema Bandari ya Dar es Salaam ni moja ya rasilimali muhimu ambazo Tanzania inapaswa kuzitumia kuongeza ushindani wa uchumi wa Taifa, akiifananisha na Mlango wa Bahari wa Hormuz kutokana na umuhimu wake kwa nchi nyingi zisizo na bahari.

Amesema kuboresha bandari, reli na barabara kutapunguza gharama za usafirishaji, kuongeza biashara za kikanda na kuifanya Tanzania kuwa lango muhimu la uchumi katika Afrika Mashariki na Kati.

Kafulila amewahimiza wasomi kuendelea kufanya tafiti na mijadala kuhusu matumizi ya PPP katika miradi ya kimkakati, akisema ushirikiano kati ya taasisi za elimu, Serikali na sekta binafsi ndio utakaowezesha Tanzania kujenga uchumi wenye ushindani, unaozalisha ajira na kuongeza ustawi wa wananchi.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI