TAASISI ya IDDEF ya Uturuki imemkabidhi Mkuu wa Mkoa Pwani Kunenge ng'ombe 500 na mbuzi 1,000 kwa ajili ya kugawia makundi yenye uhitaji kwenye sikukuu ya Eid.
Msaada huo ulioutolewa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Rahma Foundation una lengo ya kuwezesha wananchi wenye uhitaji kushiriki sikukuu hiyo kwa kuchinja kama ilivyo kwa wengine wenye uwezo.
Kunenge alisema kuwa ng'ombe hao watachinjwa na kugawanywa kwa waisalam na wasio waisalam wakiwemo yatima, wajane na wazee katika Mkoa huo.
Alisema kuwa watasimamia kwa uadilifu kwa kutatumia utaratibu wa kushirikiana na Baraza la Waislamu Tanania (BAKWATA) Mkoa wa na viongozi wa dini ili kuwafikia walengwa.
"Tunaishukuru Taasisi ya IDDEF kwa kuwezesha wananchi hao kusherekea kwa kupata kitoweo hicho kama yalivyo makundi mengine yenye uhitaji na nawaomba kwa mwaka ujao watoe tena msaada kama huu tena,"alisema Kunenge.
Kunenge alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan Kwa kuweka Mazingira bora ambapo Taasisi zimeendelea kushirikiana na Serikali kuboresha Maisha ya Wananchi.
"Tunajua Serikali haina Dini lakini Wananchi wake wana Dini, Serikali inaendelea kutoa fursa kwa Wananchi kufanya ibada,"alisema Kunenge.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Taasisi ya IDDEF Ahmad Furqan alisema kuwa wanahudumia nchi 40 za waislam na wasiokuwa Waislam.
Furqan alisema kuwa Taasisi hiyo kutoka Uturuki imeundwa kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye uhitaji kwenye nchi mbalimbali na alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusaidia Taasisi hiyo na kutoa huduma na misaada kwa watu wenye mahitaji maalumu.
Naye Mwakilishi wa Sheikh mkuu wa Mkoa wa Pwani Salmin Buda aliishukuru Taasisi hiyo kwa msaada walioutoa huku akimuahidi Mkuu wa Mkoa kushiriki kikamilifu kugawa msaada huo kwa makundi yaliyolengwa.
0 Comments