PARIS, UFARANSA.
Tanzania kupatiwa msaada wa dola milioni 25 sawa na shilingi bilioni 57 za Kitanzania kutoka kwa wafadhili wa afya ya mama na mtoto (GFF) kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto nchini.
Hayo yamebainishwa leo kwenye Mkutano wa 14 wa Global Financing Facility For Women, Children and Adolescent Health (GFF) ambapo Tanzania inawakilishwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu jijini Paris,Ufaransa.
Waziri Ummy amesema kuwa Tanzania GFF mwaka 2015/2016 ilitoa msaada kama huo kwa ajili ya afya ya mama na mtoto kiasi cha shilingi bilioni 40.
Waziri Ummy amekiambia kikao hicho kuwa Tanzania imepiga hatua katika utoaji wa hufuma za mama na mtoto na zipo dalili ya kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi na watoto.
"Tanzania ina historia ndefu ya huduma za afya za msingi,Serikali zote zilizopita hususani Mhe.Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya nne ya Jamhuri ya Tanzania aliweka mkazo mkubwa kwenye huduma za afya ya msingi".Alisema.
Hata hivyo Waziri Ummy amesema kuwa bado Tanzania ina kazi kubwa ya kufanya ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na kwa wakati hivyo amewaomba wafadhili hao kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania.
"Tunawaomba tuendelee kushirikiana ili kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto katika kipindi hiki ambacho Tanzania inajivunia kuwa na Rais wa kwanza Mwanamke Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Mkutano wa 14 wa wafadhili wa Afya ya Mama na Mtoto unafanyika jijini hapa kuanzia tarehe 6 hadi 8 Juni, 2022 ni mkutano muhimu wa wadau katika ustawi wa Sekta ya Afya na unajadili masuala mbalimbali ikiwemo uimarishwaji wa huduma za afya katika ngazi ya msingi.
Vilevile kikao hiki kinajadili changamoto zilizopo na mafanikio yaliyopatikana kupitia ufadhili wa GFF pamoja na namna bora ya kuongeza rasilimali watu kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo kuwapatia mafunzo mahususi watumishi wa afya na kuwaongezea vitendea kazi ili kuboresha huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya ngazi ya msingi.
0 Comments