Na Fatma Ally, Matukio Daima APP Dar es Salaam
Katika kuhakikisha Tanzania bara inakuza uchumi wa bluu kwa manufaa ya wananchi wote, Serikali imejipanga kupanua eneo na kukarabati Chuo cha Bahari Dar es Salaam (MDI) chuo Ili kutoa elimu yenye ubora zaidi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Eng Atupele Mwakibete wakati akifungua kongamano la kwanza kitaifa la uchumi wa bluu liloandaliwa na Chuo Cha DMI.
Amesema kuwa, Serikali inatambua eneo la chuo hicho kwa sasa ni dogo kutokana na mahitaji yaliopo hivyo imejipanga kutoa pesa kwa ajili ya kupanua na kununua baadhi ya vifaa ambavyo vimeshatumika kwa muda mrefu na kupoteza sifa.
Aidha, amewataka washiriki katika kongamano hilo kuyafanyia kazi maadhimio yatakayopatikana ikiwemo kuyafikisha kwa jamii Ili kuleta maendeleo na mabadiliko katika Sekta ya uchumi wa bluu.
"Serikali inaendelea na ununuzi pamoja na ukarabati wa meli ikiwemo meli ambayo inatengenezwa ziwa Victoria inayogharimu Sh Bilioni 90 ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 60 iweze kukamilika "amesema Eng Mwakibete.
Kwa upande wake, Balozi wa Heshima wa Seychelles nchini Tanzania, Maryvonne Pool amesema Tanzania ina maeneo makubwa sana ya bahari hivyo watumie fursa hiyo kuwekeza kwenye uchumi wa bluu waweze kufanikiwa kama nchi yao ilivyofanikiwa.
"Tuna vituo vya kufundishia huko nchini Seychelles hivyo tutasaidia baadhi ya wanafunzi waweze kufika kupata maarifa ya kutosha na waweze kuona umuhimu wa uvuvi na kutunza mazalia ya samaki "amesema Balozi Pool.
Naye, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dk Tumaini Ngurumo amesema miongoni mwa kazi zinazofanywa na chuo hicho ni pamoja na kutoa elimu, ushauri elekezi kwa vyombo vya Serikali katika masuala bahari Ili kujenga uchumi wa bluu ulioimara kwa manufaa ya nchi.
0 Comments