MULEBA.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Toba Nguvila amepiga marufuku watu wanaojimilikisha ardhi za vijiji bila kufuata utaratibu ikiwamo kuitishwa kwa mkutano wa hadhara ili wananchi waridhie, na kwamba wataobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Ilemela kata Gwanseli wilayani humo, baada ya kamati ya uchunguzi kukamilisha uchunguzi wa mgogoro wa ardhi katika kijiji hicho, na kwamba miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa ni kunyang'anywa ardhi husika.
Nguvila amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999, maamuzi ya ardhi ya kijiji ambayo inatakiwa kutumika kwa ajili ya shughuli fulani au kumilikiwa na mtu ni lazima mkutano wa kijiji ukae ufanye maamuzi na wanakijiji wasaini na kuwa na muhtasari kwa ajili ya rejea.
"Pia inabidi kutengenezwa kwa mpango maalumu wa matumizi bora ya ardhi, kwa hili ushiriki wa wananchi ni muhimu ili waweze kufahamu ni mipango ipi imepangwa kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi ya kijiji" amesema Nguvila.
Ametoa mfano kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi utakaowekwa na kupitishwa, kuwa eneo la njia ya mifugo ni marufuku mtu mwingine kuliziba, kwa sababu njia za mifugo zinapozibwa ndio chanzo cha migogoro ya wafugaji na wakulima.
Ripoti ya kamati ya uchunguzi iliyosomwa na mchunguzi kutoka jeshi la polisi Wilaya ya Muleba, Inspekta Joseph Dishon, kuhusiana na mgogoro wa ardhi katika kijiji cha Ilemela, imebaini kuwa vyanzo vya migogoro huo ni kutofuatwa kwa Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999.
Inspekta Dishon amesema kuwa baada ya kubaini vyanzo vya migogoro hiyo kamati ilipendekeza masuala mbalimbali ili kukabiliana navyo ikiwamo
serikali ya kijiji kutambua maeneo yake na kuyawekea ulinzi ili kuepusha kuvamiwa na wananchi wenye uchu wa ardhi bila kufuata utaratibu.
"Serikali ya kijiji pia iunde kamati maalumu ya kubainisha ardhi zilizorudishwa pamoja na ardhi ambazo umiliki wake haukuwa halali, ili ziweze kuwekwa vizuri kwenye kumbukumbu ya ardhi ya kijiji pamoja na kuweka mipaka ya kudumu" amesema.
Pia kamati hiyo ilishauri waliojimilikisha ardhi kinyume na utaratibu warudishe ardhi hizo kwenye serikali ya kijiji na ardhi zitakazorudishwa zitambuliwe ili ziwekwe kwenye orodha ya ardhi wazi za kijiji.
Mwisho









0 Comments