Header Ads Widget

MKUU WA WILAYA YA NAMTUMBO AIPONGEZA KAMPUNI YA MANTRA TANZANIA .

 




Na Amon Mtega, Namtumbo.


MKUU wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Dkt Julius Ningu ameipongeza kampuni ya Mantra Tanzania Limited inayojishughulisha na madini aina ya Uranium   yaliyomo Wilayani humo kwa kushirikiana na Wananchi kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwenye jamii.


Mkuu huyo amezitoa pongezi hizo alipotembelea banda la maonyesho la kampuni hiyo kwenye maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi (MEI MOSI)mwaka huu ,ambapo kimkoa zimefanyika Walayani  humo huku mkuu huyo amekuwa mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.


 Dkt Ningu akiwa kwenye banda hilo amesema kuwa kampuni ya Mantra Tanzania Limited imekuwa mstari wa mbele kuwa karibu na Wananchi wa Wilaya hiyo kwa kutatua changamoto mbalimbali hivyo ni vema wakazi wa maeneo hayo kuendelea kuunga mkono jitahada hizo.



Kwa upande wake Meneja uhusiano wa kampuni hiyo Khadija Pallangyo amesema kuwa kampuni hiyo hadi sasa imeweza kutoa misaada mbalimbali kwenye jamii katika nyanja za Elimu,Afya, Michezo pamoja na mafunzo ya usalama barabarani kwa Vijana madereva boda boda pamoja na kwa Wanafunzi ambao shule wanazosoma zipo mazingira ya kwenye barabara kuu ya Namtumbo -Tunduru na shule zilizopo barabara ya Likuyusekamaganga ambayo inaelekea kwenye eneo la madini ya Uranium .


 Meneja uhusiano huyo  amefafanua kuwa kampuni hiyo imekuwa bega kwa bega na wakazi wa Wilaya hiyo katika suala zima la maendeleo na kutatua changamoto mbalimbali  ambazo huwa zinajitokeza kwenye jamii.


Hata hivyo Pallangyo ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano unaofanyika kwenye Kampuni hiyo pamoja na kufanya maendeleo mbalimbali kwa Wananchi wake.


Ikumbukwe hivi karibuni Kampuni ya Mantra Tanzania Limited imetoa msaada wa bati zenye thamani ya Milioni 10 kwenye kaya zaidi ya 100 zilizopatwa na maafa ya mvua iliyoambatana na upepo mkali katika Kijiji Cha Likuyusekamaganga .

    


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI