Header Ads Widget

ATHARI YA MABADILIKO YA TABIA NCHI YABADILI MFUMO WA HALI YA HEWA

 


Na Fatma Ally Matukio Daima APP, Dar es Salaam


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema athari za mabadiliko ya tabia nchi katika mifumo ya hali ya hewa imesababisha kutokana na kuvurugika kwa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kuathiri mwenendo wa unyeshaji wa mvua za Masika, 2022.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi amesema hali hiyo imetokana na mabadiliko ya muda mfupi ya joto la Bahari ambayo ni nadra kutokea kutokana na tabia ya Bahari kutunza joto au baridi kwa muda mrefu.


Amesema kumekuwepo kwa vipindi virefu vya ukavu vilivyojitokeza katika kipindi cha mwezi Machi, 2022 hususani kwa eneo la Pwani ya Kaskazini na nyanda za juu Kaskazini Mashariki ambapo maeneo hayo yalipata mvua chache.


Hata hivyo, amesema mwenendo wa vimbunga na mabadiliko katika joto la Bahari vimechangia Ukandamvua (ITCZ) kuendelea kusalia katika maeneo ya kusini mwa nchi ambapo kwa kawaida katika kipindi cha mwanzoni mwa mwezi Machi huanza kuelekea maeneo ya Kaskazini mwa nchi.


"Hali hiyo imesababisha kuvurugika kwa mwenendo wa mifumo ya bali ya hewa na kuathiri mwenendo wa unyeshaji wa mvua za Masika, 2022,” amesema  Dkt. Kijazi.


Sambamba na hayo, amesema katika kipindi kilichosalia cha msimu wa masika 2022, mifumo ya hali ya hewa inaashiria kuongezeka kwa joto la bahari Mashariki mwa bahari ya Hindi pamoja na kupungua kwa joto la Bahari Magharibi mwa  Bahari ya Hindi katika Pwani ya Afrika Mashariki na hivyo kupunguza upepo wenye unyevunyevu kuvuma kuelekea katika maeneo ya nchi.


Amesema hali hiyo inatarajiwa kusababisha mvua za Masika 2022, kuwa za chini ya wastani hadi wastani katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mara, Simiyu, na Shinyanga.


Aidha ameeleza kuwa mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa kuendelea katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza pamoja na maeneo ya Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma (Wilaya ya Kibondo na Kakonko).


Aidha, amesema kumejitokeza mabadiliko ya muda mfupi ya joto la Bahari katika eneo la Pwani ya Afrika Mashariki na eneo la Mashariki mwa Bahari ya Hindi.


"Ingawa maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani katika msimu huu wa mvua za Masika 2022, izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza,” ameeleza Dkt. Kijazi.


Dkt. Kijazi amebainisha mvua zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya kwanza nay a pili ya mwezi wa Mei 2022 katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini na kuisha kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi wa Mei 2022, katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS