Na THABIT MADAI, ZANZIBAR.
WAKATI Taifa likijiandaa kuingia katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Imeelezwa kwamba Waandishi wa Habari ndio kundi muhimu katika kuhamasha jamii kujitokeza kuhesabiwa na upatikanaji wa takwimu sahihi.
Hayo yameelzwa na Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe Wakati akizungumza na Waandishi wa Habari huko Maru Maru Mjini Unguja.
Amesema kuwa, Waandishi wa Habari wanatakiwa kuwa Mstari wa kuhamasisha jamii kujitokeza kwa Kuhesabiwa ili kupatikane kwa takwimu sahihi na kufanikisha zoezi hilo.
Aidha ameeleza kuwa Waandishi wa Habari wanapaswa kushajihisha jamii kuwatoa watu wenye Ulemavu ili waweze kuhesabiwa katika Sensa ya Watu ns Makaazi.
“Waandishi wa Habari wanapaswa kutusaidia ili kupata takwimu sahihi za Watu wenye Ulemavu katika kipindi cha Sensa ya Watu na Makaazi ya mwaka 2022,” alieleza.
Hata hivyo alifahamisha kuwa Takwimu sahihi za Watu wenye Ulemavu zitasaidia Serikali kupanga vyema Mikakati ya Kuwasaidia Watu wenye Ulemavu Nchini.
Mkurugenzi Debe amesema,zipo changamoto katika takwimu zinazohusu watu wenye ulemavu ambapo kwa Sasa kiwango kikubwa ni ulemavu wa uoni ambao unakisiwa kuwa na watu wapatao 27,000 wakifuatiwa na watu wenye ulemavu wa usikivu ambao ni 15,000.
Aidha amesema zipo Aina nyingi za ulemavu ambao unaendelea kuwakabili watu mbali mbali hapa Zanzibar kama vile ulemavu wa viungo, ulemavu wa akili, ulemavu wa kujihudumia na ulemavu wa ngozi (albino).
Kwa Mujibu Sensa ya Watu na Makaazi ya mwaka 2012 inaonesha kuwa Zanzibar ina Idadi ya Watu Milioni 1.5 huku Watu Wenye Ulemavu wapatao 75,000 ambao sawa na Asilimia 5.
Mwisho......
0 Comments