Header Ads Widget

UMMY MWALIMU MAPOKEZI YA CHANJO YA SINOVAC UWANJA WA NDEGE

 



Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na afya hadi kufikia siku ya leo na kuweza kujumuika tena hapa katika tukio hili muhimu la mapokezi ya Chanjo dhidi ya UVIKO-19. Pili, shukrani za pekee ziwaendee wadau wetu wa Maendeleo hususani katika kujali afya za Watanzania kwa kuendelea kutupatia chanjo ambazo zitatusaidia kuwakinga wananchi dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19). 


Kwa niaba ya Serikali chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunaishukuru Serikali ya Uturuki kwa kupokea ufadhili wa chanjo aina ya Sinovac, jumla ya dozi 1,000,000 kati ya dozi 4,000,000 zinazotarajiwa kupokelewa kwa awamu nne. Chanjo hizi zinatarajiwa kuchanja watu 2,000,000. Nichukue fursa hii kuishukuru Serikali ya Uturuki kwa kuwezesha upatikanaji wa chanjo hizi. Hii ni mara ya kwanza kwa nchi yetu kuanza kutumia chanjo aina ya Sinovac tokea zoezi la uchanjaji lilipozinduliwa rasmi na Mhe Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 28 Julai,2021.


Mapokezi ya chanjo hizi za leo yanafanya jumla ya chanjo tulizopokea nchini tangu tuanze kutoa chanjo dhidi ya UVIKO 19 hadi sasa kuwa dozi 10,845,774 zikijumuisha (Sinopharm, Janssen, Moderna,Pfizer na Sinovac), ambazo zinatosha kuchanja watu 6,381,327.



Serikali itaendelea kutoa Chanjo dhidi ya UVIKO-19 katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za Afya hapa nchini kwa mujibu wa miongozo iliyopo zikiwemo huduma za mkoba na tembezi. 


Hadi kufikia tarehe 21 Marchi, 2022 jumla ya watu milioni 3,016,551 wamepata chanjo kamili kati ya watu milioni 30,740,928  wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ikiwa ni sawa na asilimia 9.81.


Ninachukua fursa hii kuendelea kuwasisitiza viongozi na watendaji wa ngazi zote kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kuhimizwa kwenda kwenye vituo vya huduma za afya ili wakapate elimu kuhusu umuhimu wa chanjo na kisha kuchanja. 



Aidha, ninawahimiza wananchi kuendelea kuchukua hatua mbalimbali za kujikinga dhidi ya UVIKO-19 ikiwa ni pamoja na uvaaji wa barakoa, kunawa mikono kwa maji na sabuni, kutumia vipukusi (sanitizer) na hatua nyingine ambazo wataalamu wa afya wamekuwa wakiendelea kuzisisitiza.




Katika kufikia kinga jamii dhidi ya UVIKO 19, Serikali inalenga kuchanja asilimia 70 ya Watanzania kuanzia umri wa miaka 18 hadi kufikia mwisho wa mwaka 2022. 


Hivyo basi, ninatoa rai kwa Wakuu wa Mikoa yote nchini kuongeza juhudi za uhamasishaji jamii ili kuongeza kiwango cha utoaji wa chanjo na kuhimiza wananchi wakapate chanjo kama inavyoshauriwa na wataalamu. 


Aidha, ninawahamasisha watoa huduma za afya katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini, wao wenyewe wachanje, na ninawaagiza waendelee kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wahudumu wa afya ngazi ya jamii, wajumbe wa kamati za afya ya msingi na viongozi mashuhuri wakiwemo viongozi wa dini na kimila.




Vilevile, ninawaelekeza wataalamu kujumuisha huduma za chanjo ya UVIKO 19 sambamba na huduma nyinginezo za afya zikiwemo huduma za uzazi wa mpango, VVU, tohara, macho, lishe, na kifua kikuu.


Ninawaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuendelea kuongeza vituo vya kutolea chanjo ili kuendelea kusogeza huduma hizi karibu na wananchi. 


Niendelee, kuwasihi Wananchi,wajitokeze kwa wingi kwenda kupata chanjo na waendelee kuchukua tahadhari zote za kinga dhidi ya UVIKO-19 zikiwemo kunawa mikono na maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi, kuvaa barakoa katika maeneo yenye misongamano, kuepuka misongamano isiyokuwa ya lazima, kula mlo kamili na kufanya mazoezi kila mara.


Mwisho, Nitumie fursa kuwathibishia wananchi kuwa chanjo hizi ziko salama na mpaka sasa chanjo ndiyo njia pekee iliyothibika kupunguza madhara yatokanayo na janga hili la kidunia. 


Pia, nishukuru nchi mbalimbali ambazo zimeendelea kutupatia msaada wa chanjo za UVIKO-19 katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kupambana na ugonjwa huu.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



BBC NEWS