Header Ads Widget

UMAHIRI WA MACHIFU WAKINYAKYUSA IV

 


Adeladius Makwega-DODOMA


Mwanakwetu katika matini iliyotangulia juu ya umahiri wa machifu wa Kinyakyusa kulikuwa na maswali makubwa matatu.


Kwanza, kwa nini Chifu Merere, Mwandangala (Mngoni) na Viongozi wa Wahehe waliweka mezani ajenda za kuteka wanawake wa Kinyakyusa na kupora mifugo na kuondoka nayo? 


Kulijibu swali hili ni kwamba Mwandangala ambaye alikuwa Mngoni, miongoni mwa Wangoni hao walitokea huko Afrika ya Kusini alikuwa na uzoefu wa vita, kwa desturi ya sehemu kubwa ya safari zao walikuwa ni askari kwa hiyo waliweza kupigana pahala popote na walipopita waliweza kuoana na wanawake wa kabila lolote, kwa kuwa mtoto anayezaliwa alikuwa na ukoo wa baba.


Kwa hiyo kama wamewateka wanawake wa Kinyakyusa basi Wangoni wangekuwa na ujamaa na Wanyakyusa na hivyo ingekuwa mbinu nyengine ya kuwazoofisha Wanyakyusa.


Kwa hoja ya mifugo, ifahamike wazi mifugo ya Wanyakyusa ilikuwa imenawili sana, kwa hiyo hilo lingewasaidia Wangoni chini ya Mwandangala kuwa na mifugo ambayo hapa awali hawakuwanayo kwa maana kwa sehemu kubwa walikuwa vitani huku Wasangu na Wahehe wangejiongezea mifugo hiyo kama mali na wakati huo huo kama chakula chao.


Swali la pilli, Je Wasangu, Wahehe na Wangoni hawakuwa na wanawake wazuri? Kwa hakika Wasangu walikuwa na wanawake kadhaa pamoja na Wahehe lakini lengo la kuteka nimelieleza hapo juu ili kuwazoofisha Wanyakyusa na kuingia katika imaya yao ni kusaidia kuzaa nao na kuwapa nguvu zaidi Wangoni ambao katika eneo hilo walikuwa wageni


Swali la tatu , kwanini machifu hao wakubwa walizijadili ajenda hizo na kuwa mpango wa vita hivyo? Ajenda hizo zilijadiliwa kwa kina kwa kuwa ilikuwa mbinu mbadala kama wangeshindwa vita hivyo mara baada ya kuwavamia Wanyakyusa.


“Vita vilianza kupiganwa mno na kwa hakika Wanyakyusa walipigwa vilivyo. Zoezi hilo liliambatana na kutekwa mifugo na wanawake. Kazi hiyo ilifanyika vizuri katika muunganiko huo wa Mandangala, Wasangu na Wahehe.”


Haya yanathibitishwa na J S Mwakipesile katika maandiko yake ya utani kwa kabila la Wanyakyusa. Sasa ilikuwa tayari eneo kubwa na Wanyakyusa, mifugo na wanawake kadhaa imeshatekwa.


Askari wa umoja huo wakakaribia eneo la Rungwe ya kati hapo mapambano yalikuwa makali mno . Wanyakyusa walikuwa wamejipanga vilivyo kupamba na wavamizi hao.


Hapa Wanyakyusa walipambana kufa na kupona na hadi tamati Wangoni na washirika wake walifurushwa mbali huku kila mmoja akitafuta njia ya kutoka katika eneo hilo.


Wangoni walichanganyikiwa zaidi hata hawakukumbuka kurudi tena kwa Chifu Merere hapo ndipo wakaelea Malawi. Lakini Chifu Merere na Viongozi wa Wahehe walibahatika kukimbia na mifugo mingi na mateka kadhaa ambapo wakati walipoteka walikuwa wakiondoka nao na kuwahifadhi katika maeno kadhaa nje ya imaya ya Wanyakyusa.


Ndiyo maana inaaminika hata mfugo kadhaa iliyopo kwa Wasangu na wahehe ni masalia ya mifugo hiyo ya Wanyakyusa. Hata mateka hao waliondoka nao ndiyo maana hata sasa unaweza kuwakuta watu kadhaa maeneo ya Wahehe na Wasangu wakiwa na majina ya Kinyakyusa kama vile Mwakalinga, Mwangata ambao yana asli ya Unyakyusani.


Hao ni baadhi ya wale waliongukia mikononi mwa Wangoni, Wahehe na Wasangu katika vita hivyo.


Mwandangala mwenyewe aliuwawa katika vita hivyo huko Rungwe katika eneo linalofahamika kama Selya na kuzikwa katika eneo linalaofahamika kama Njanga. Inaaminika watu wengi walifariki katika vita hivyo huku Wanyakyusa wakipeana taarifa kuwa popote anapooneka Msangu Mhehe au Mngoni auwawe.


Taarifa za kuwasaka ndugu hao ilisikika lakini shida ilikuwa ni kumtambua Mngoni.Wasangu na Wahehe walikuwa wakifahamika vizuri, Iliaminika kuwa Wangoni walikuwa wakila chakula ambacho hakijapikwa na jambo hilo ndiyo ilikuwa ishara ya kuwatambua ndugu hao.


Wangoni wengine walijificha msituni hadi hali ilipotengemaa ndipo walipojitokeza mathalani masali yaoa wapo katika maeneo ya Masukulu na Ipinda Inaaminika jamaaa hawa wanazungumza mno Kiswahili na Kinyakyusa cha kubahatisha bahatisha  tu huku Kingoni hawakifahamu kabisa.


Ndiyo kusema hapo ndipo ukawa utani baina ya Wanyakyusa na Wangoni, Wanyakyusa na Wahehe na Wanyakyusa na Wasangu hadi leo.


Je kipi kitaendelea subiri matini ijayo.


Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com

0717649257

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI