Header Ads Widget

TANZANIA KUSHIRIKIANA NA WADAU KUTENGENEZA VYANDARUA VYENYE DAWA KWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA KISASA



NA WAF-DODOMA


Serikali kupitia Wizara ya afya imetoa wito kwa wawekezaji wa nje kuwekeza nchini katika kutengeneza vyandarua vyenye dawa kwa teknolojia ya kisasa (New Generation Nets) kwa kusaidiana na wawekezaji wa ndani hatua inayotajwa kuwa itasaidia kubadilishana ujuzi na kusaidia mapambano dhidi ya maambukizi ya Malaria.


Hayo yamesemwa leo tarehe 2 Machi, 2022 na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Bi. Joy Phumaphi ambaye ni Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Umoja wa Marais wa Afrika katika mapambano dhidi ya Malaria (ALMA) katika ofisi za Wizara zilizoko Mtumba jijini Dodoma.


Katika mazungumzo hayo ambayo yalilenga kuona namna gani ya kukabiliana na ugonjwa wa Malaria,  Waziri Ummy amemwambia Bi. Joy kuwa hatua hiyo ya uzalishaji wa vyandarua vyenye dawa vitakavyotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa itasaidia kukabiliana na usugu wa mbu dhidi ya dawa aina na Paleto ambayo inatumika kwenye vyandarua hivi sasa.


Pamoja na mengine Waziri Ummy amemwambia Bi. Joy kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuanzishwa kwa baraza la kutokomeza Malaria ikiwa ni mkakati mmojawapo wa kukabiliana na Malaria ambapo uzinduzi wake utafanyika katika kilele cha siku ya maadhimisho ya Malaria duniani tarehe 25 Aprili 2022.



Kwa upande wa takwimu za mwenendo wa Malaria nchini, Waziri Ummy amesisitiza kuendeleza matumizi ya Scorecard ambapo ametoa wito kwa mabaraza ya madiwani pamoja na viongozi wa ngazi ya jamii katika kuhamasisha jamii iweze kuwa na uelewa wa matumizi ya kitendea kazi hicho ambacho kinatoa taarifa muhimu zitakazowezesha kupata takwimu na kuwezesha utatuaji wa changamoto za huduma za afya ngazi ya jamii.


Kwa upande wake Bi. Joy ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na taasisi za kimataifa pamoja na wadau wa maendeleo katika kutekeleza afua mbalimbali zinazoratibiwa na taasisi hizo na kumuahidi Mhe. Waziri kuwa ALMA itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya na sekta ya afya kwa ujumla ili kukabiliana na ugonjwa wa Malaria ambao bado unaendelea kuwa tishio kwa nchi nyingi za kiafrika.




Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI