Header Ads Widget

SIMAMIENI KWA WELEDI MIRADI INAYOENDELEA KATIKA MAENEO YENU.

 



NA NAMNYAK KIVUYO,_ARUSHA.



Viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali halmashauri ya Meru ikiwemo hospitali na shule wametakiwa kusimamia kwa weledi miradi mbalimbali inayoendelea katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaohitajika.



Wito huo umetolewa na mjumbe wa kamati ya siasa ya halmashauri kuu CCM mkoa wa Arusha Robert Kaseko kwa niaba ya mwenyekiti wa chama hicho Mkoa katika ziara ya kukagua miradi mbalimbali  inayoendelea katika halmashauri hiyo kuelekea mwaka mmoja tangu serikali ya awamu ya sita kuingia madarakani ambapo alisema kuwa Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu amekuja na mpango wa ustawi wa maendeleo ya taifa na jukumu lao ni kuhakikisha miradi inayotokana na mpango huo wanaisimamia vizuri na kwa weledi wa hali ya juu.



Akikagua jengo la wagonjwa wa dharura linalojengwa katika hosipitali ya wilaya ya Meru Kaseko alieleza kuwa katika ujenzi huo wamepewa milioni 300 na ameona kazi inayoendelea ni nzuri na jengo linajengwa katika ubora wa hali juu tofauti na ilivyokuwa ikienea katika mitandao ya kijamii kuwa jengo hilo limetelekezwa na hakuna kinachoendelea.


“Niseme tu kwamba zile ni siasa chafu, mtu  ambaye anataka kuona nini kinafanyika afike mwenyewe saiti kwani sio utani kazi ni nzuri inayofanyika hapa wameanza Februari 10 na wanatarajia kukamilisha Aprili 15, wamefunga taa hadi kwenye miti kuashiria kuwa kazi inafanyika masaa 24 na kwa hatua waliyofikia na ni jengo kubwa mimi sina wasiwasi,”Alisema Kaseko.



Aidha akiwa katika shule mpya ya sekondari ya Ambureni alisema kuwa kama kuna mambo ya kujivunia aliyoyafanya Rais Samia ni pamoja na mapinduzi aliyoyafanya katika sekta ya Afya na elimu ambapo katika elimu ametambua nini maana ya Elimu bure kwani ameboresha sekta hiyo kiasi kwamba hakuna mtoto yoyote mwenye sifa ya kwenda shule atakayebaki nyumbani kutokana na uhaba wa madarasa wala madawati.


“ Lakini katika ujenzi wa majengo haya katika shule hii mpya ya Ambureni ipo haja ya nyie mafundi  kuongeza nguvu kazi ili kuweza kukamilisha mradi huu wa milioni 470 kwa wakati  lakini pia viongozi na wananchi mliopo hapa kuitumza miradi hii vizuri ili iweze kuwanufaisha wanafunzi waliopo sasa na watakao kuja miaka ijayo,” Alisisitiza.




Katika shule ya sekondari Sin'gisi aliwataka wanafunzi pamoja na walimu kuhakikisha wakati wote wanatunza miundombinu ya majengo ya madarasa waliyojengewa ili yawe endelevu kwa vizazi vijavyo lakini pia amewaeleza kuwa Rais Samia yupo pamoja nao katika kuhakikisha anawatengenezea mazingira mazuri ya kujifunza na kufundishia.




Kwa upande wake Afisa elimu taaluma mkoa wa Arusha Shirley Swai kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela alisema kuwa ujenzi wa miundombinu ya hosipitali inayoendelea itasaidia kusogeza huduma za afya zenye ubora karibu na wananchi lakini pia miundombinu ya shule itaondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu jambo lililokuwa na madhara hasa kwa wanafunzi wa kike kwa kuwa chanzo cha kupata mimba.


Aidha aliwataka wananchi wanapofanya mipango miji wahakikishe wanatenga maeneo kwaaji ya kujenga vituo vya kutolea huduma kama vile zahanati, shule na mengineyo kwasababu watu wanoongezeka lakini eneo linabaki kuwa lile lile ambapo maeneo ambayo wameshayatenga na tayari yameshaanza ujenzi kwaajili ya huduma wahakikishe yanakuwa na hati miliki ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza hapo baadae.




Naye diwani wa kata ya Akeri Julias Mungure alisema kuwa katika kata hiyo Mh. Rais amewapa fedha nyingi katika miradi mbalimbali ikiwemo shule, hosipitali, maji na barabara ambapo fedha hizo sio tu zinaleta maendeleo ya kimiundombinu lakini pia wananchi mmoja mmoja wamekuwa wakinufaika kutokana na manunizi ya vifaa yanayoendelea katika kata hiyo.



Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI