MTU mmoja amefariki na wengine watatu kujeruhiwa baada ya Polisi Kigoma kufyatua risasi upande wa mashabiki waliokuwa uwanjani kufuatia ghasia zilizozuka kati ya mashabiki wa Mwandiga FC vs Kipampa wakati wa mechi ya fainali za kuwania ngo'mbe na kombe la Dr. David Livingstone kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma ambapo Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma, James Manyama alisema katika kudhibiti vurugu hizo, Askari walitumia mabomu ya machozi na mabomu ya kishindo kudhibiti mashambuliano baina ya mashabiki hao lakini vurugu ziliendelea na kusababisha Askari mmoja kupigwa mawe kichwani na kuanguka akiwa na silaha ya AK 47.
"Wakati akiwa chini Askari huyo akijihami kunyang’anywa silaha na kutetea uhai wake alifyatua risasi tisa hewani akitoa onyo kwa kuwatawanya mashabiki ambao waliendelelea kumshambulia kwa mawe, ndipo alifyatua risasi tatu ambazo kwa bahati mbaya zilimpata Shabiki Juma Ramadhani(35) ambaye alijeruhiwa pajani na nyingine ikampata Omary Amdani (35) aliyejeruhiwa unyayoni na ya tatu ilimjeruhi Nasibu Moshi(35)"
Aliyefariki ni Juma Ramadhani(35) na amefariki wakati akiendelea na matibabu katika Hosptali ya Mkoa Maweni Kigoma na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kigoma maweni kwa ajili ya uchunguzi.
Polisi Kigoma wanawashikilia Watuhumiwa wanne ambao wanatuhumiwa kuwa chanzo cha vurugu hizo na upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea na Watuhumiwa hao watafikishwa Mahakamani kwa hatua za kisheria
0 Comments