Na Shemsa Mussa -Matukio Daima.
Kagera.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendesha kura za maoni za kuwapata wagombea ubunge katika majimbo mbalimbali nchini leo Agosti 4, 2025, ambapo Jimbo la Missenyi limemshuhudia Florent Kyombo akiibuka mshindi kwa kishindo. Kyombo amepata kura 2,979 kati ya kura zote zilizopigwa, na kuongoza kwa tofauti kubwa dhidi ya wapinzani wake.
Katika matokeo yaliyotangazwa na msimamizi wa kura hizo, Projestus Tegamaisho ameshika nafasi ya pili kwa kura 1,355, akifuatiwa na Assumpta Mshama amepata kura 475. Washiriki wengine ni Plasidius Ndibalema (166), Naswiru Byabato (88), Jacklyne Rushaigo (52) na Amina Athuman (9).
Ushindi wa Kyombo unatajwa kuwa matokeo ya ushawishi wake mkubwa kwa wananchi wa Missenyi na historia yake ya kushirikiana na jamii katika shughuli za maendeleo. Baadhi ya wanachama waliokuwa wakishuhudia kura hizo wamesema ushindi huo ni ishara ya kuaminiwa kwa uongozi wake na matarajio ya kuona maendeleo zaidi jimboni humo.
Kura za maoni za CCM ni hatua muhimu katika mchakato wa kupata mgombea rasmi wa ubunge atakayewakilisha chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu ujao. Hatua inayofuata ni mchakato wa chama kuthibitisha majina ya washindi na kuwatangaza rasmi kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubunge kupitia tiketi ya CCM.
0 Comments