Na Matukio Daima Media Dar.
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) linamshikilia ALLEN SAMWEL MHINA, ( 31) Mkurugenzi wa Mtandao wa kijamii wa U-turn Collection mkazi wa Temeke Mwembeyanga na wenzake 13 kwa tuhuma za kusambaza video katika mitandao ya kijamii kinyume na sheria.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ACP Muliro J Muliro mapema leo ametoa taarifa kwa umma mbele ya Waandishi wa habari ambapo ambainisha kuwa:
"Mtandao huo wa kijamii hivi karibuni ulirusha maudhui ya video ikimuonyesha mmoja wa wagonjwa aliyekuwa amelazwa wodi ya ICU Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,
Jeshi hilo limesema suala hilo liliweza kuleta taharuki kwa Hospitali hiyo na wafanyakazi wake.
"Watuhumiwa hao walikutwa na vifaa mbalimbali vya kieletroniki vya kiuchunguzi ambavyo ni Kamera, Kalamu, Saa, funguo, Miwani, Kofia, Laptop, Memory Card ambavyo vyote vinachunguzwa." Alisema Kamanda Muliro Muliro.
Na kuongeza kuwa:
"Kitendo kinachotuhumiwa kufanywa na watuhumiwa hao kililenga kudhalilisha, kutia hofu au kuleta taharuki suala ambalo linalazimisha mamkala hizi mbili za kisheria kuchunguza kwa kina suala hilo. Uchunguzi ukikamilika watafikishwa kwenye vyombo vingine vya kisheria." Alimalizia Kamanda Muliro Muliro.
Hata hivyo, mtandao huu wa Matukio Daima uliripoti tukio hilo kwa mara ya kwanza juu ya kukamatwa kwa watu hao waliofahamika kufanya kazi katika mtandao wa Mange Kimambi kupitia Mange Kimambi App ambao hivi karibuni walirusha maudhui kinyume na sheria yakimuonesha Joseph Haule 'Prof. Jay msanii maarufu na mwanasiasa ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Mikumi, Mkoani Morogoro.
Mwisho.
0 Comments