Na, Mwandishi wetu- BUKOBA
Katika ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa shule mpya za Sekondari (SEQUIP) kwa Kata ambazo hazikuwa na shule ya sekondari, Kata ya Mushabago na Kata ya Mafumbo pamoja na upanuzi wa Kituo cha Afya cha Kamachumu kwa fedha za Tozo, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila amewataka mafundi waliopewa kazi za ujenzi kuongeza kasi ya ujenzi kwakuwa fedha zipo kwenye akaunti hivyo hakuna sababu inayowafanya kuchelewesha kumaliza miradi hiyo.
Akizungumza na mafundi hao na wajumbe wa kamati za ujenzi, ameeleza kuwa anaridhishwa na kiwango cha ujenzi ila kasi iongezwe kwakuwa malengo ya Serikali ni kuhakikisha baada ya likizo fupi za mwezi Aprili watoto wote wanaotoka katika kata zao warudi kusoma katika shule zilizojengwa ndani ya kata yao.
"Tarehe 30.03.2021 natarajia nikabidhiwe majengo, sitarajii kufikia tarehe hiyo kwamba kuna watu mtakuwa hamjakamilisha ujenzi.Naagiza vifaa vyote vya ujenzi viwe eneo la ujenzi kwani fedha zipo hivyo kusiwepo sababu ya kuchelewesha kazi," ameeleza Mhe. Nguvila
Sambamba na hilo ameagiza kuwa kuanzia sasa kazi ifanyike masaa 24, kwani kwa siku zilizobaki atafanya ziara za mara kwa mara ili kuona kama maelekezo yake yamezingatiwa. Huku akielekeza kuwa kila jengo wawepo mafundi nane na vibarua 8.
Aidha, amewataka mafundi wakuu kuwasimamia mafundi wao na sio kuondoka eneo la kazi kila wanavyojisikia huku wakiacha ujenzi haundelei hali inayopelekea kutomaliza kazi kwa wakati. Na kuagiza mafundi wakuu ambao hakuwakuta katika eneo la mradi shule mpya ya sekondari ya kata ya Mushabago, wakaripoti kituo cha Polisi cha Kamachumu na kutoa maelezo kwanini wameondoka eneo la ujenzi bila kutoa taarifa kwa kamati ya ujenzi.
Afisa Takukuru (w), Said Lipunjaje amezishauri kamati za ujenzi kuhakikisha vifaa vyote vinakuwepo eneo la ujenzi. Na kuwashauri mafundi kuzingatia mipango kazi yako na sio kujenga tu, hii itawasaidia kila fundi na kibarua kuwajibika kwa pamoja.
Diwani wa Kata ya Mushabago Mhe. Aaron Mpumbya kwa niaba ya wananchi wa Kata ya Mafumbo amemshukuru sana Mkuu wa Wilaya na wataalam kwa kutochoka kufika katika kata yao ili kuona ujenzi unavyoendelea na kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa pamoja wa namna ujenzi huo unavyokwenda, hii inasaidia hata kasoro inapojitokeza inakuwa rahisi kurekebisha kabla ya ujenzi kufika mbali.
Naye Ansbert Sabinian, Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi shule mpya ya sekondari ya Mafumbo amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuwatembelea mara kwa mara, kutoa ushauri na kushirikiana nao katika ujenzi huo jambo ambalo linaonesha ni uwajibikaji wa viongozi kwa jamii.
Mhe. Nguvila amewapongeza wasimamizi na kamati za ujenzi, kwa kusimamia kwa karibu na kuhakikisha ujenzi unaenda kwa kasi. Na kusisitiza Kamati za Ujenzi kuhakikisha vifaa vyote vya ujenzi kama sementi, nondo, mawe, mbao, mchanga na kokoto vinakuwepo eneo la ujenzi.
Miradi iliyotembelewa na kukaguliwa ni ujenzi wa shule mpya ya Mushabago kwa gharama ya Tsh. milion 470, ujenzi wa shule mpya ya sekondari kata ya Mafumbo kwa gharama ya Tsh milioni 470 na upanuzi wa kituo cha Afya cha Nshamba kwa gharama ya Tsh 250.
0 Comments