NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tamisemi David Silinde, akiongozana na Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini Prof Patrick Ndakidemi,walifanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya Daraja la Rau, mradi wa Ujenzi wa Kituo Cha Afya Uru Kusini, pamoja na mradi wa ujenzi wa Jengo la Halmashauri ya Moshi linalojengwa eneo la Sango, Kata ya Kimochi.
Katika mradi wa daraja la Rau umeshamilika na imebakia kuweka lami pande zote mbili liweze kupitika vizuri ambapo kwa sasa wananchi wameshaanza kutumia daraja hilo.
Naibu Waziri amemtaka mkandarasi amalize kazi mapema kusudi liweze kuzinduliwa mapema iwezekanavyo ambapo ujenzi wake mpaka kukamilika utagharimu kiasi cha Shilingi milioni 910.
Naibu Waziri huyo alielekea kata ya Uru Kusini ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Afya Uru Kusini ambapo hivi karibuni serikali imetoa Shilingi milioni 250 awamu ya kwanza kuendeleza shuguli za ujenzi ulioasisiwa na nguvu za wananchi, Chama cha ushirika na halmashauri ya Moshi.
Silinde amewataka wahusika wote wasimamie vyema ujenzi na uendane na thamani ya pesa iliyotolewa huku pia akitaka ujenzi uende kwa kasi kwani fedha zipo na ujenzi huo uko nyuma wa muda.
Naibu Waziri Silinde ameahidi kuwa serikali italeta fedha nyingine milioni 250 kukamilisha ujenzi.
Aidha Naibu Waziri huyo alikagua jengo la Halmashauri ya Moshi ambapo mkandarasi ni SUMA JKT na kuisifu safu nzima ya viongozi wa Halmashauri kwa kazi nzuri inayoendelea.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Moshi Kastori Msigala alimhakikishia Naibu waziri kuwa mradi wa ujenzi utakamilika mwezi October mwaka huu ambapo mpaka kukamilika utagharimu kiasi Cha Shilingi bilioni 2.2 ambapo mpaka sasa Serikali kuu imeshaleta kiasi Cha Shilingi bilioni 1.78.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, Prof Patrick Ndakidemi ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo miradi ya barabara, afya, elimu, maji, umeme, maendeleo ya jamii na kilimo.
Vilevile, Mbunge Ndakidemi alimshukuru sana Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa kwenye jimbo la Moshi vijijini kwani ziara hiyo imewapa wananchi hamasa na kujisikia kupendwa na serikali yao.
Aidha mbunge ameiomba serikali iendelee na nia njema ya kutekeleza miradi mbalimbali jimboni, ikiwemo ile iliyoainishwa kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri Silinde aliongozana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Moshi, Angelina Marko, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Moshi na madiwani wa kata za Uru Kusini, Uru Mashariki, na Kimochi, pamoja na viongozi mbali mbali wa Chama na Serikali
Mwisho....
0 Comments