Adeladius Makwega-DODOMA.
Mama huyu alipokuwa mgonjwa alipoona hali yake ni mbaya aliamua kurudi nyumbani kwao huko Zanzibar angalau kuweza kuugulia jirani na wazazi wake. Kwa hiyo aliwaagiza watoto wake wafunge milango ya chumba chake vizuri na yeye kupelekwa bandarini kupanda boti la Zanzibar.
Safari hiyo ilikuwa ngumu, kwani abiria katika boti hilo wakilaumu kwanini wanamsafirisha mtu mgonjwa aliyezidiwa?
Lawama hizo zilikuwa sawa na kutia sindano ya moto katika kidonda kibichi.
Hoja hiyo haikuwa na maana yoyote kwa mama huyu mgonjwa lakini pia hata kwa watoto wake kwani mama huyu alikuwa anarudi nyumbani kulinda utu wake. Akiamua kwenda kumalizia muda uliobakia wa uhai wake kwao ambapo mama yake angemsaidia kwa siku zilizosalia japokuwa mama yake alikuwa mzee sana.
Mama huyu alikuwa na watoto wa kiume saba na hakujaliwa mtoto wa kike, kwa hiyo ilikuwa ngumu vijana hao kumsadia katika huduma zote katika hali ya ugonjwa huo.
Jambo hilo lingekuwa jepesi kama watoto wake wangekuwa na wake lakini walikuwa bado hawajajaliwa kuoa.
Mama huyu katika kipindi chote cha ugonjwa, majirani na nduguze katika imani waliokoa jahazi hilo lakini ilihitaji mtoa huduma aliyejirani zaidi. Kwani majirani hawa walikuwa na shughuli zao za kila siku.
Mgonjwa alifikishwa kwao na kupokelewa na kuuguzwa na baba na mama yake. Nyumbani kwao waliuguza kwa majuma matatu tu na kufariki dunia, mazishi yalifanyika huko huko kwao huku majirani wa Dar es Salaam tukijulishwana wengine kushiriki.
Mara baada ya mazishi vikao vilikalika, wasimamizi wa mirathi hiyo wakichaguliwa. Lakini kumbuka mama huyu kabla ya kifo alifunga chumba chake.
Vijana wa mama huyu walirudi Dar es Salaam lakini nguo za mama yao wanazipeleka wapi? Chumba hicho kimefungwa na funguo hazionekani.
Chumba cha mama huyu kilivunjwa na watu kadhaa kuingia wakiwamo akina mama majirani wawili. Akina mama hawa waliombwa kuzikusanya nguo hizo na kuzifunga katika marobota.
Robota la Mabegi, Robota la Viatu, Robota la Magauni, Robota la Khanga, Robota la Vitenge, Robota la Nguo Ndogondogo, Robota la Suti na Sanduku Dogo la Vidani.
Tulipofika katika Sanduku Dogo la Vidani, mzee mmoja alishauri kuwa vidani hivyo vitambuliwe aina ya kidani, aina ya madini yake na vihesabiwe na orodha yake iwekwe ndani ya sanduku na nakala ibaki kwa mjumbe.
Hapo mwanakwetu nikapewa kazi ya kuyatambua madini hayo, nilipewa kazi lakini mwanakwetu nimejifunzia wapi kuyatambua madini? Wazee wakikupa kazi na njia ya kuifanya wanakupa.
Nilikabidhiwa sanduku dogo, kazi yangu ni kuingiza mkono na kunyanyua juu. Wao wanasema hiyo ni pete ya dhahabu. Mie naandika ya kwanza pete ya dhahabu. Nikaingiza mkono tena hii. Wakajibu mkufu wa dhahabu, Mie nikaandika pili mkufu wa dhahabu. Kazi ilikuwa hivyo na nyepesi hadi mwisho.
Tulipomaliza sanduku lilifungwa na funguo moja na nakala ya vitu vyote alibaki nayo mjumbe na funguo moja na orodha ya vitu vilipelekwa msikitini na nakala nyengine alipewa mtoto wa mama huyu kwenda nayo Zanzibar
Binafsi niliitazama mizigo ile ilivyokuwa katika marobota na sanduku dogo. Nikajiuliza namna maisha ya binadamu yalivyo.
Nikajiuliza je binadamu anaweza kuvaa jozi mbili za suti kwa wakati mmoja?
Je binadamu anaweza kuvaa jozi mbili za viatu kwa wakati mmoja?
Jibu lake lilikuwa hapana.
Nikasema yule mwenye jozi mbili za suti na mwenye jozi moja ya suti wote wamevaa. Yule aliyelala katika gorofa na yule aliyelala katika nyumba ya mbavu za mbwa na makuti, wote wamelala usingizi.
Nilibaini kuwa katika maisha binadamu anahitaji kupata mahitaji yake ya msingi kwa kiasi tu na nilibaini kuwa duniani hakuna wa jozi mbili kwa wakati mmoja bali sote ni wa jozi moja kwa wakati mmoja.
Mwanakwetu majirani tulipakiza marobota yale na sanduku lile ndani ya gari kuelekea huko bandarini na kupakizwa botini hadi Zanzibar.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments