Na Fatma Ally MDTV Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Eliamani Sedoyeka amesema Serikali haiwezi kupiga hatua katika Sekta ya elimu bila kupokea mawazo mapya yenye takwimu kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo Shirika la Haki Elimu.
Kauli hiyo ameitoa jijini Dar es Salaam wakati alipokua akizindua ripoti ya utafiti kuhusu elimu ya afya ya uzazi na haki kwenye shule za msingi na Sekondari Tanzania bara ambao umeandaliwa na Shirika la Haki Elimu kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa elimu.
Amesema kuwa, Serikali inatambua mchango wa wadau wa elimu ambao umekua ukitolewa katika Taasisi mbalimbali hivyo, wataendelea kushirikiana nao Ili kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Hata hivyo, amesema Serikali ipo katika mchakato wa kupitia sera, sheria na kanuni za elimu pamoja na miongozo mbalimbali hususani mitaala ya elimu, huku akiwataka wadau kufanya utafiti utakaokwenda kutoa matokeo chanya hususani katika masuala ya afya ya uzazi .
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Haki Elimu, Dkt John Kalage, amesema matokeo ya utafiti huo yalioongozwa na wataalamu yameonesha bado kuna changamoto zinazohitaji kufanyiwa kazi Ili elimu ya afya ya uzazi na haki iwe yenye tija.
"Mfano, kwa mujibu wa matokeo asilimia 15 pekee ya wanafunzi waliohojiwa waliridhika na utoshelevu wa maudhui ya elimu ya afya ya uzazi na haki, ambapo asilimia 93.3 ya walimu walisema maudhui ya elimu ya afya ya uzazi na haki hayatoshelezi huku asilimia 33.3 walimu wamesema maudhui hayo hayafai kufundishwa"amesema Dkt, Kalage.
Aidha, amesema kuwa utafiti huo umefanyika katika mikoa ya Dodoma, Lindi,Rukwa, Mara na Arusha huku ukizingatia kanuni zote ambapo mikoa iliyochaguliwa kwa makusudi ya kupata uwakilishi wa kijiografia wa Kanda kuu za nchi na kuzingatia Takwimu za utafiti wa Taifa wa kidemografia na hali ya afya - Viashiria vya malaria (TDHS - MIS).
Hata hivyo, amesema lengo kuu la utafiti lilikua ni kuchunguza uzingatiaji wa elimu ya afya ya uzazi na haki katika mfumo wa elimu msingi Tanzania Bara, ambapo ulilenga kuchunguza uwepo wa sera, sheria na miongozo ya elimu ya afya ya uzazi na haki za jinsia katika shule za msingi na Sekondari.
Naye, Mkurugenzi kutoka Taasisi Damas Solution Mwemezi Ngemela amesema ni muhimu wadau kuendelea kutetea na kuwekeza kwenye elimu ya afya ya uzazi na haki za jinsia nchini Ili kuhakikisha wanafunzi hasa wasichana na wavulana wanafaidika na elimu hiyo.
Amesema kuwa, matokeo ya utafiti huo yanaonesha elimu ya afya ya uzazi na haki za jinsia imewaacha wasichana walio katika madarasa ya chini ya shule ya msingi kutokana na wasichana wengi hubaleghe katika umri mdogo, hivyo imependekezwa elimu hiyo itolewe kuanzia madarasa ya chini zaidi.
0 Comments