Na Mwandishi Wetu
MGANGA mkuu wa Serikali, Dkt. Alifeo Sichalwe ametoa neno katika maadhimisho ya wiki ya figo duniani.
"Tanzania leo inaungana na mataifa mengine Duniani katika kuadhimisha siku ya Figo ambayo huadhimishwa kila Alhamisi ya Wiki ya Pili ya Mwezi Machi. Mwaka huu, Wiki hii inaadhimishwa kuanzia Tarehe 7 mpaka 11 Machi, 2022 na leo Alhamisi tarehe 10, 2022 ikiwa ni siku ya Figo Duniani.
Kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa mwaka huu ni “Afya ya Figo kwa Wote", ambayo inalenga kuhamasisha afya ya figo kwa wote.
Lengo kuu likiwa ni kuongeza elimu na ufahamu wa Afya ya figo na kuwahamasisha wananchi kujitokeza kupima Afya zao mapema kabla figo hazijaathirika na kupoteza uwezo wa kufanya kazi.
Pia, kupitia maadhimisho haya tunatafakari mikakati ya udhibiti wa magonjwa ya figo katika ngazi zote za utoaji wa huduma za Afya.
"Figo ni kiungo muhimu sana mwilini na hufanya kazi nyingi, ikiwa ni pamoja na kuondoa uchafu na maji ya ziada kutoka kwenye Damu (Kutengeneza Mkojo) ambayo hatimaye hutumika kuondoa uchafu mwilini.
Pia Figo hufanya kazi nyingine mwilini ili kuwezesha mwili kufanya kazi ipasavyo.
Figo zako: Hudhibiti kemikali mbalimbali zinazohitajika na zisizohitajika mwilini, pia zina kazi ya kudhibiti shinikizo la juu la Damu, vilevile husaidia kudumisha Afya ya mifupa pamoja na kusaidia utengenezaji wa chembe hai nyekundu za damu.
"Ugonjwa sugu wa figo huchangiwa kwa kiasi kikubwa na Magonjwa Yasiyoambukiza kama ugonjwa wa kisukari, shinikizo la juu la damu na maambukizi kama virusi vya UKIMWI na virusi vya homa ya ini.
Pia matumizi mabaya au holela ya dawa mbalimbali ikiwa ni pamoja na antibiotics.
"Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa asilimia 10 ya watu wote duniani wanaishi na ugonjwa sugu wa figo. Tatizo ni kubwa zaidi kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 75 ambapo asilimia 50% ya watu hao wana ugonjwa wa Figo.
"Vilevile, tatizo hili ni kubwa kwa wanawake ukilinganisha na wanaume ambapo ugonjwa huu hutokea kwa mwanamke 1 kati ya 4 ukilinganisha na kutokea kwa ugonjwa huu kwa wanamme ambapo takwimu zinaonesha kuwepo kwa mwanamme 1 kati ya 5 wenye umri kati ya 65 mpaka 74 kuishi na ugonjwa wa figo.
Tafiti zinaonyesha kuwa kati ya asilimia 11 hadi 17 ya watu wote wanaoishi Afrika hususan kusini mwa jangwa la Sahara wana ugonjwa wa figo.
" HapaTanzania kupitia utafiti uliofanyika mwaka 2013 katika jamii ulionyesha kuwa asilimia 7 ya watanzania wanaishi na ugonjwa wa figo.
Wagonjwa wengi wenye tatizo la figo pia walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa kisukari na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
" Tutafanya utafiti wa viashiria vya Magonjwa Yasiyoambukiza mwaka huu 2022, na tunatarajia kupata takwimu zitakazosaidia kufahamu hali halisi ya vichocheo vya magonjwa ya figo nchini.
Tafiti zimebaini kuwa takriban Watanzania 5800 mpaka 8500 wanahitaji huduma ya kusafisha damu yaani dialysis au huduma za kupandikizwa figo.
"Hadi kufikia Januari 31, 2022 wagonjwa 2750 sawa na asilimia 32 wanapata huduma ya kusafishwa damu (dialysis) na wagonjwa 325 wamepandikizwa Figo.
" Vilevile, Kati ya wagonjwa waliopandikizwa figo; wagonjwa 93 wamepandikizwa nchini, ambapo, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imepandikiza wagonjwa (67) na Hospital ya Benjamin Mkapa Dodoma imepandikiza wagonjwa (26).
"Huduma za figo hususan za usafishaji wa damu (dialysis) zimekuwa zikitolewa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, pamoja na hospitali za Kanda na Hospitali Maalum. Katika mkakati wa kupanua huduma hizi Serikali imeendelea kuzijengea uwezo Hospitali za Rufaa za Mikoa kutoa huduma za dialysis.
Hadi sasa, awamu ya kwanza ya utekelezaji imekamilika ambapo serikali imeanzisha huduma za uchujaji damu (dialysis) kwenye hospitali za Mikoa 7 kwa kuzipatia mashine 49 za dialysis na kukarabati majengo kwa gharama ya Tsh bilioni 2.8.
" Hospitali za Rufaa za Mikoa zilizoanzisha huduma hizi ni Hospitali za Mikoa za Mtwara, Arusha, Tanga, Kigoma, Kagera, Mara na Mwanza Sekou Toure ambapo mpaka sasa wagonjwa zaidi ya 150 wameweza kufaidika na huduma hizi.
"Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan imeanzisha awamu ya pili ya upanuzi wa huduma katika hospitali nyingine 12 ambapo mpaka sasa mashine za dialysis 110 na mashine za kuchakata maji 11 zimeanza kusimikwa katika Hospitali husika.
Jumla ya TZS bilioni 4.9 zitatumika kujenga vituo 4 vipya vya dialysis na kukarabati majengo 7 katika Hospitali hizo. Hospitali hizo ni hospitali za Mikoa za Songea, Morogoro, Mwananyamala, Temeke, Amana, Tumbi, Mawenzi, Chato, Dodoma, AICC-Arusha na Mbeya.
Mipango iliyopo ni kwamba Ifikapo Juni, 2023 hospitali zote za Rufaa nchini zitakuwa zikitoa huduma za usafishaji damu (dialysis) na hivyo kusogeza huduma hii karibu na wananchi ,hivyo kuongeza kiwango cha watu wanaofanyiwa dialysis kutoka asilimia 32 ya sasa hadi kufikia asilimia 50 ifikapo June 2023.
Niwashukuru sana MSD na NHIF kwa kuwa mshirika na mdau mkubwa wa utekelezaji wa mpango huu ambao pamoja na kupanua huduma tunaamini kuwa utaenda kupunguza pia bei ya huduma za dialysis kwa wagonjwa.
Kwa sasa kipindi kimoja cha kusafisha damu ni TZS 300,000 na mgonjwa huhitaji vipindi vitatu kwa wiki ambapo gharama inakuwa laki 9, kwa mwezi milioni 3.6 na kwa mwaka milioni 43.2 kwa mgonjwa mmoja.
Ni Watanzania wachache sana wanaweza kumudu gharama hizi. Nimeambiwa kuwa Mkakati huu mpya unaoihusisha MSD na NHIF utaenda utapunguza gharama hizo kwa zaidi ya asilimia 50 na hivyo kuwezesha watanzania wengi kumudu gharama.Niwapongeze sana na niwaombe muongeze kasi ya utekelezaji wa mkakati huo.
Nimeambiwa hapa kuwa Hospitali ya Tumbi ambayo ipo katika awamu ya pili inaendelea vyema kuhakikisha huduma za dialysis zinaanza kutolewa mapema iwezekanavyo. Ukarabati wa jengo la huduma ya kusafisha damu unaendelea na watumishi wanaendelea na mafunzo katika Hospitali ya Mlongazila.
Mashine mpya 10 za kusafisha damu na mashine 1 ya kuchakata maji zimeshafika hapa Tumbi na ukarabati utakapokamilika zitasimikwa. Dkt Malima na Timu yako hongereni sana kwa hatua hii. Mimi ninawatakia kila la kheri.
Pamoja na kuimarisha huduma za matibabu ya magonjwa ya figo nchini, Serikali imejipanga kuweka jitihada za kipekee ili kuzuia na kudhibiti ugonjwa figo na magonjwa yasiyoambukiza kwa ujumla kwa kuimarisha afua za kinga kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba.
Hapa naomba nikumbushe umuhimu wa kubadilisha mtindo wa Maisha kwa kuhimiza ufanyaji wa mazoezi, kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, kupunguza matumizi ya pombe , vile vile kuzingatia ulaji wa mlo kamili wenye mboga mboga na matunda ya kutosha ili kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa.
Pia, kupunguza matumizi yachumvi, sukari na vyakula venye mafuta mengi, pamoja na kuzingatia unywaji wa maji ya kutosha angalau kiasi cha lita 1.5 ya maji kwa siku au bilauri/glasi 8 kwa siku.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni
“Afya ya Figo kwa Wote”. Kauli mbiu hii inalenga kuhimiza kila mwananchi kufahamu vizuri ugonjwa wa figo na kila mmoja kuthamini afya ya figo zake kwani Magonjwa ya figo yanatuhusu sisi sote.
Sote tunahitaji kufahamu umuhimu wa Afya ya figo na kuchukua hatua Madhubuti za kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wenye ugonjwa wa figo.
Kama nilivyokwisha sema hapo awali,serikali imefanya maboresho makubwa kwenye miundombinu ya afya, vifaa na vifaa tiba, kusomesha na kuajiri watumishi wenye elimu na ujuzi wa juu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora karibu na maeneo yao.
Lakini ili kila mwananchi aweze kupata huduma bora bila kikwazo chochote, ni lazima kila mmoja wetu awe na Bima ya Afya.
" Ukiwa na bima ya afya utaweza kupima afya yako muda wowote, ukiugua wewe au mwananafamilia utatibiwa wakati wowote. Kukosa Bima ya Afya ni sawa na kukosa uhakika wa matibabu, hakuna aneyejua ataumwa lini, saa ngapi na tatizo lake litakuwa la ukubwa gani, hivyo sio rahisi kuwa na fedha za kulipa papo kwa papo. Magonjwa yasiyoambukiza hususan ni magonjwa sugu ya figo yana gharama kubwa na pia ni ya muda mrefu sana, ukisema ulipie papo kwa papo itafika wakati utashindwa au utauza mali zako kwa ajili ya matibabu.
" Nawasihi sana wananchi kateni bima za Afya ili muwe na uhakika wa matibabu pamoja na familia zenu.
"Nipende kuweka msisitizo kwa kila mmoja wetu kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa sugu ya figo kwa kufanya yafuatayo.
" Kurekebisha ulaji wa vyakula kwa kuongeza ulaji wa mbogamboga, matunda na kupunguza vyakula vyenye mafuta mengi, chumvi na sukari.
" Kufanya mazoezi angalau dakika 30 mara tano kila wiki. Hapa niweke msisitizo kwa sekretarieti za mikoa na Mamlaka za serikali za mitaa kuendeleza utaratibu wa mazoezi uliozinduliwa na Mheshimwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan wakati akiwa Makamu wa Rais.
"Utaratibu wa kuwa na vikundi vya mazoezi unasaidia sana kuleta hamasa ya kufanya mazoezi.
"Kupunguza matumizi ya vilevi hususan pombe, tumbaku na bidhaa zake.
Kuwa na utaratibu wa kupima afya kila mara ili kuweza kupata matibabu mapema kabla ugonjwa haujaleta madhara makubwa.
"Niombe pia timu za Mikoa na halmsahuri kusimamia na kuhakikisha kuwa vituo na Halmshauri zinaweka katika bajeti zake huduma za magonjwa yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja na uchunguzi wa figo.
"Naomba kuwashukuru wadau wote waliochangia na kufanikisha maadhimisho haya ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hapa uwanjani.
" Pia, napenda kuwapongeza watoa huduma wote hapa uwanjani kwa kazi nzuri ya kuwahudumia wananchi na mwisho uongozi wa Mkoa wa Pwani kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya Kitaifa, na kwa namna ya pekee niwapongeze sana kamati ya maandalizi kwa kazi nzuri waliyoifanya.
"Ndugu zangu baada ya kusema hayo ninawaasa mzingatieni mitindo bora wa maisha ili kuimarisha Afya njema ya figo kwaj wote.
0 Comments