.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amezielekeza mamlaka za maji nchini kuketi meza moja na wadai sugu wa maji ili wakubaliane namna ya kulipa kidogokidogo madeni wanayodaiwa.
Waziri huyo amesema njia hiyo itakua ni bora kuliko mamlaka hizo kuendelea kuwasitishia ama kuwakatia wateja hao sugu huduma.
Aweso amesema hayo wakati Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea na kukagua miradi ya maji ikiwemo wa Mlandizi -Chalinze - Mboga inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Dawasa).
"Naomba mamlaka zote za maji mkakae na wananchi hasa wale wadaiwa wetu sugu namaanisha wenye madeni ili muangalie kwa pamoja namna gani wataweza kulipa madeni waliyonayo bila kukatiwa maji"amesema Aweso
Kuhusu huduma ya kuunganishia wateja wapya maji, Waziri huyo ameitaka Dawasa na Ruwasa kuacha ubabaishaji wa kuwambia watu vifaa havitoshelezi kwani wananchi wanachokitaka ni maji na mamlaka hizo zipo kwa ajili hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Dk Christina Ishengoma ameishukuru Dawasa kwa kuusimamia mradi wa maji wa Mlandizi - Chalinze -Mboga na kuweza kumaliza kwa wakati kwani unawapa fursa wananchi wa Chalinze na maeneo jirani kupata huduma ya majisafi na salama.
0 Comments