Teddy Kilanga, Arusha
Baadhi ya Wenyeviti wa mitaa katika kata ya Levolosi wamesema zoezi la uhakiki wa anwani za makazi limeenda vizuri kwani wananchi wamekuwa na uelewa wa kutosha kutokana na elimu waliyopatiwa na wataalamu wa halmashuri ya jiji kwa kushirikiana viongozi mbalimbali.
Akizungumza februari 16,2022 baada kukamilisha kwa siku ya pili ya zoezi hilo walisema mwanzoni lilikuwa na changamoto za wananchi kutokutoa ushirikiano lakini leo limeenda vizuri hali ambayo imewarahisishia utendaji kazi wao.
Mwenyekiti wa mtaa wa Levolosi,Eveline Shirika alisema zoezi la urasmishaji anwani za makazi ambapo zoezi hilo lilianza februari 15,2022 japo changamoto zilizokuwepo siku ya kwanza zimetuliwa na leo limeenda vizuri.
"Leo ni siku ya pili ambapo zoezi hili limeenda vizuri ikiwa idadi ya nyumba zimeongezeka hivyo tunashukuru wananchi kwa kusaidia kufanikisha jambo hili kwani wanatoa ushirikiano mzuri,"alisema Mwenyekiti huyo.
Naye Mratibu wa zoezi hilo katika kata ya Levolosi,Haliye Abubakari alisema wako katika siku ya pili ya utendaji wa kazi hiyo ambapo leo wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwani changamoto zilizokuwepo hapo awali zimepungua kwa kiasi kikubwa.
"Ukizingatia jana tulipitia jumla ya barabara 11 na nyumba 120 katika huu mtaa wa Levolosi lakini leo wamefikia barabara 18 pamoja na nyumba 127 kwani haya ni mafanikio makubwa wa uendeshaji wa zoezi hili,"alisema Mratibu.
Baadhi ya waendesha bodaboda waliishukuru serikali kwa kuanzisha anwani za makazi hali ambayo itasaidia kuendesha shughuli zao za usafiri kwani wanapitia changamoto ya wateja wageni kuelewa majini ya mitaa lakini zoezi hilo likikamilika litawaondolea adha hiyo.
0 Comments