Adeladius Makwega-DODOMA
Kutokana na maendeleo ya sayansi na tekinolojia hivi sasa Watanzania wengi wanafanya shughuli zao katika maeneo mbalimbali ndani ya jumuiya kadha wa kadhaa kama vile viwandani, maofisini, masokoni na maeneo kadhaa ya watu wa jamii mbalimbali.
Katika mikusanyikio hiyo kuna watu wa dini tofauti, makabila tofauti na ndani yake utani ni mojawapo ya jambo linalofanyika kila mara, huku shughuli za msingi za ndugu hao zikifanyika, huu ni UTANI MGUDINI (Gudi ni pahala kazi inapofanyika mathalani bandarini, sokoni, kazini na kadhalika)
Utani huu hufanyika katika makundi makubwa manne. Utani wa kabila na kabila, utani wa wanaume na wanawake, utani wa kubuzibuzi na utani wa michezo.
Mwaka 1991 nikiwa mwanafunzi wa Tambaza niliwahi kumtembelea rafiki yangu mmoja anafahamika kama Ibrahimu Liguo huko Manzense, mara nyingi nakusimulia habari zake katika matini zangu. Ndugu huyu tuliambatana naye hadi Kiwanda cha Nguo cha Urafiki, hapo baba yake mzazi alikuwa akifanya kazi.
Tulipofika getini kiwandani hapo Ibrahimu alijitambulisha kwa walinzi na baada ya muda baba yake alifika na kuongea nasi.
Watumishi wanzake mzee huyu walipokuwa wanapita tulipokaa walimtania.
“Kumbe una watoto wakubwa kabisa, sasa hivi utaitwa babu.”
Wafanyakazi wa kiwanda hicho walitaniana bila woga, hilo lilinipa picha kuwa mzee huyu alikuwa akielewana na wafanyakazi wenzake.
Miaka tisa baadaye nilitembelea kiwanda hicho, tena nikiwa na mama yangu mzazi, hapo tulienda kumchukua binti mmoja wa mjomba wangu ambaye alitokea huko Kondoa.
Wafanyakazi wa kiwanda hiki walimtania mama yangu wakisema kuwa mama vipi tema unaacha binti huyu huko Ujombani muda wote huo kwanini? Wewe ni shangazi yake ebo! Utakosa ng’ombe mama.
Huku aliyemleta binti huyo tukiambatana naye. Akiwaambia wafanyakazi wenzake waache vurugu kwa wageni wake. Hii pia lilinipa picha kama ile ya mwaka 1991.
Aina hii ya utani inaenda mbali hadi inawaingiza Watanzania wenye asili ya Bara Asia kwa kuwatania namna wanavyongea na mambo kadhaa baina yao.
Hapo utani huu haufanywi Wahindi na Waarabu kama wageni, bali wanakuwa ndugu wa jamii husika. Hapo ndipo misemo, nahau na methali kadhaa zinaibuka.
“Baniani mbaya, kiatu chake dawa.”
Aina ya nyengine ya utani wa mgudini ni ule wa wa baina wa wanaume kwa wanawake.
Utani huu wa makazini ni mkubwa sana. Wanaume namna walivyo huwa ni wazungumzaji wa habari za watu kwa kupiga makelele, bila aibu.
Katika vikao vyaoa huzungumzia uzuri wa mwanamke fulani namna alivyo, maumbile yake na kama ynaywavutia au laa.Anaweza kupita mwanamke na maeno kadhaa yanaweza kutamkwa mathalani.
“Mashallah !, Hongera !, Mungu Fundi !, Kaumbika! ,Yarabi Nafsi ! Masalale ! La lawhaula la Kwata ! na mengine mengi.”
Huku wanaume wengine wakitoa milio ya sauti kama vile kuguna, miluzi nakadhalika kuonesha ishara ya utani huo kwa mwanamke.
Japokuwa vitendo hivyo vilifanyika au vinafanyika kandoni kuna sheria ya makosa ya kujamiiana.(SOSPER). Mwanakwetu kuwa makini jambo hilo akipelekewa mheshimiwa hakimu mezani anaweza kuzamisha jahazi.
Kwa upande wa wanawake jambo hili huwa kwa siri sana lakini linazungumzwa mno na tena vikao vyao huwa vya muda mrefu sana kuliko vikao vya wanaume.
Wanawake huyazungumza haya kwa muda mrefu sana na ndiyo maana wanaume wenye desturi ya kuwataka wanawake kimapenzi katika maeneo ya kazi au kwenye mijumuiko ya watu wengi hujulikana kwa haraka mno na mwisho siku hukataliwa kwani siri hiyo haiwezi kukaa na mwanamke mmoja bali wanasimuliana katika vikao vyao.
“Mie amenitaka, hata mie amenitongoza, hata Jane, ehh hata Aisha, hata Mariam na Joyce naye, ah huyu anataka kutuchezea tu, piga chini huyo.”
Mwisho wa siku muugwana huyo ataishia kusimuliwa vibaya tu na wala hawezi kuila nyama japokuwa kisu anacho.
Aina ya tatu ya utani mgudini ni ile ya kubuzibuzi, hapa wafanyakazi hao huwa wanapanga miadi kadhaa ya kukutana huku wakinywa pombe, kwenye VIcoba na mikusanyiko mingine baada ya kazi. Utani huu unafanyika hasa kati ya tarehe za mishahara kama vile 21-30-31 na hata 1-5 hapa waliowengi huwa na fedha za kwenda kufanya vikao hivyo.
Utani huu ni mara chache mno unafanywa na wanawake wenyewe kwa kuweka mijadala ya kukutana bali huwa baina ya wanawake na wanaume, hukutana na kupiga soga hizo. Katika utani huu wale Walevi Komba huwa hawatakiwi, kwani wakati wa mazungumzo haya wanakuwa wameshalewa.
Basi mwanakwetu kwa leo naishia hapo , matini ijayo nitamalizia na utani michezoni.
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
0 Comments